DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Monday, January 06, 2014

RC DODOMA AWASISITIZA WALEMAVU KUANZISHA MIRADI YA UFUGAJI NYUKI

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi akiwasisitiza wajumbe wa Chama cha Walemavu Tanzania-CHAWATA mkoa wa Dodoma kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki ili kujiongezea kipato wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hiko uliofanyika jana mjini Dodoma.

Baadhi ya wanachama wa Chama cha Walemavu Tanzania-CHAWATA mkoa wa Dodoma wakisikiliza kwa makini salamu za Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho uliofanyika jana mjini Dodoma.

Katibu wa Chama  cha Walemavu Tanzania-CHAWATA mkoa wa Dodoma Ndg. John Mlabu akielezea changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu mkoani Dodoma wakati akiwasilisha risala ya chama hicho kwa Mkuu wa Mkoa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (watatu) wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika jana mjini Dodoma.


Pichani ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma  Dr. Rehema Nchimbi (katikati) na wanachama wa Chama cha Walemavu Tanzania-CHAWATA mkoa wa Dodoma muda mfupi baada ya mkuu huyo wa mkoa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hiko uliofanyika jana mjini Dodoma.
..........................................

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi ameziagiza wilaya zote mkoani humo kuhakikisha zinatenga ardhi kwa ajili ya watu wenye ulemavu na kusisitiza kuwa ardhi hiyo ni lazima ipimwe na kutolewa hatimiliki. Aidha, ametaka ardhi hiyo itakayotengwa kwenye kila wilaya itumike kujengea ofisi za chama cha walemavu Tanzania Ngazi za wilaya na kufanyia miradi ya uzalishaji ili kujipatia kipato.

Vilevile Dr. Nchimbi alitoa rai kwa Chama cha Walemavu Tanzania-CHAWATA mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanaanzisha miradi ya ufugaji nyuki ambayo wataifanyia kwenye ardhi watakazopatiwa na wilaya.

Dr. Nchimbi aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa mwaka wa CHAWATA mkoa wa Dodoma ambapo aliwatia moyo walemavu kwa kuwaeleza kuwa miradi ya ufugaji nyuki katika mkoa wa Dodoma imeonesha kufanya vizuri na soko zuri lipo ndani na nje ya Nchi. Aidha, Alieleza kuwa ufugaji nyuki hauhitaji fedha nyingi na wala haumhitaji mtu kwenda kushinda kwenye mradi kila siku akifanya kazi badala yake nyuki wenyewe ndio wanafanya kazi ya uzalishaji, jambo ambalo lina manufaa sana kwa watu wenye ulemavu.

Aliahidi serikali kutoa msaada wa usimamizi na utaalamu katika miradi hiyo ya nyuki ambapo ameagiza Maafisa Ustawi wa Jamii mkoa na wilaya kusimamia miradi itakayoanzishwa na Maafisa Nyuki wa wilaya wahakikishe wanahudumia miradi hiyo upande wa utaalamu. Pia, amezitaka Halmashauri za Wilaya kuhakikisha zinaweka miundombinu ya usimamizi ikiwa ni pamoja na kugharamia gharama za wasimamizi wa miradi hiyo.


Dr. Nchimbi alimaliza kwa kuwaasa CHAWATA kuwa mapato ya miradi hiyo ya nyuki yatumike kugharamia gharama za uendeshaji wa shughuli za CHAWATA ili walemavu waendeshe shughuli zao bila kutegemea kuomba misaada, vilevile mapato hayo yanaweza kutumika katika miradi mingine zaidi ya uzalishaji na hivyo kuwanyanyua walemavu mkoani Dodoma.

Nae Katibu wa CHAWATA mkoa wa Dodoma Ndg. John Mlabu akiwasilisha taarifa ya chama chake kwa kueleza kuwa zipo changamoto nyingi zinazowakabili ikiwemo ukosefu vyumba vya ofisi za wilayani. Kwani Halmashauri nyingi hazitengi bajeti kwa ajili ya walemavu,  walemavu kutotengewa maeneo ya biashara kwenye maeneo yanayoainishwa kufanyia biashara na gharama za visaidizi mwendo (magongo, wheelchairs na tricycle) kuwa juu.

Nyingine ni bei kubwa za viwanja vinavyouzwa na Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu-CDA ambapo walemavu hawawezi kuzimudu na vilevile majengo mengi hasa maghorofa na baadhi ya ofisi nyeti hayajazingatia miundombinu ya watumiaji walemavu.

No comments:

Post a Comment