Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania –TRL unachukua fursa hii kuwataarifu wateja wetu wote na Watanzania kwa ujumla na hasa ukanda wa ziwa kuwa hatimaye ile huduma iliyokuwa ikisubiriwa leo Aprili 12 , 2015 inaelekea Mwanza 'Rock City' Ziwa Victoria!
Safari hii ni ya pili kwa vile ya uzinduzi iliyofanyika Aprili Mosi , 2015 ilielekea Kigoma Ziwa Tanganyika baada ya kuzinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Dk Shaban Mwinjaka. Aidhaa taarifa zinaeleza kuwa treni hiyo ilipokelewa kwa furaha na bashasha sehemu zote ilimopita wakati wa kwenda Kigoma na kurudi Dar es Salaam.
Tayari kuna baadhi ya wakazi wa miji njiani wameutaka Uongozi wa TRL kuiruhusu treni hiyo ya Deluxe isimame katika vituo zaidi vya njiani zaidi ya vile rasmi 14 na vile vitatu vya ufundi.
Hata hivyo msharti ya uendeshaji wa huduma hii ya Deluxe unaifunga kama ilivyotolewa na Sumtra unaifunga TRL kuchukua uamuzi wa upande mmoja kwa vile uamuzi wowote hautakiwi kuathiri muda wa safari na viwango vya huduma ambazo msafiri wa Deluxe amehakikishiwa kimkataba.
Aidha safari za deluxe zitakuwa wiki mara moja siku za Jumapili itaondoka Stesheni ya Dar es Salaam saa 2 usiku ikiwa na mabehewa 15, Daraja la kawaida 10 (abiria 80 kila moja) daraja la pili la kukaa 3 (kila moja abiria 60) na daraja la pili kulala 2( kila moja watu 36). Itasimama katika vituo 17 ambavyo ni pamoja na Morogoro, Kilosa, Dodoma, Makutopora, Saranda, Manyoni, Aghondi, Itigi, Tabora, Urambo, Kaliua, Uvinza, Kigoma. Vituo vingine ni Isaka, Shinyanga, Malampaka na Mwanza. Wiki moja ikienda Kigoma wiki inayofuatia itaenda Mwanza.
Kwa wasafiri wa Dodoma na Tabora hawa watatumia huo usafiri wakati wote isipokuwa wale wanaoishia Kigoma na Mwanza. Siku za usoni wakati mabehewa mengine ya deluxe yatapatikana safari zitakuwa kila wiki kwenda Kigoma na Mwanza.
NAULI ZA TRENI YA DELUXE KWA MUHTASARI KUTOKA DAR KWENDA KIGOMA/MWANZA NIA KAMA IFUATAVYO:
Dar -Dodoma daraja la kawaida TZS 18,500, Daraja 2 Kukaa TZS 24, 700 Kulala: 41,200
Dar -Tabora kawaida 25,400, Daraja la 2 Kukaa 33,900 Kulala 56,500;
Dar - Kigoma kawaida 35,700, Daraja la 2 Kukaa 47,600 na Kulala 79,400 na
Dar - Mwanza ;kawaida 35,000, Daraja la 2 kukaa 46,700 na Kulala 77,800.
Aidha pia tunapenda kutoa wito wa ushirikiano wa wananchi na wadau wote kutunza vitendea kazi na kwamba kila mmoja awe mlinzi wa mwenziwe. Tujiepushe na vitendo vya makusudi kuharibu mabehewa haya mazuri ndani na nje . Kuna msemo : KITUNZE KIDUMU'! Tukitunza vitendea kazi vitaweza kutoa huduma kwa muda mrefu na hivyo kuongeza tija na kupunguza matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.
Imetolewa na Afisi ya Uhusiano ya TRL kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.
|