Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda (Mb), amekataa ombi la wakazi wa jimbo lake la uchaguzi la Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango ya maendeleo aliyoianzisha.Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari ilimnukuu Pinda akijibu maombi ya wakazi hao baada ya Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Dar es Salaam . (Picha na Fadhili Akida)Pinda alisema anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya ubunge wa Jimbo la Katavi. Alisema ataendelea kuwa karibu na wakazi wa jimbo hilo wakati wote na kwa vile atakuwa na muda wa kutosha kushiriki kikamilifu katika mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wajikwamue kutoka kwenye umaskini. Kwa upande mwingine, Pinda aliwaasa wakazi wa jimbo hilo wawe makini kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Akimshukuru Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani humo, Padri Aloyce Nchimbi, aliwaasa wakazi wa Mlele kumuenzi Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na uzoefu wake katika kujiletea maendeleo. Pinda yuko kijijini kwake Kibaoni ajili ya mapumziko mafupi na alitoa msimamo wake huo jana ikiwa ni siku ya mwisho kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa na kupokea fomu kwa makada wake wanaoomba wateuliwe kugombea ubunge na udiwani katika uchaguzi huo utakaovishirikisha pia vyama vya upinzani.Msimamo huo wa Pinda umekuja siku chache baada ya jina lake kukatwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM hivi karibuni mjini Dodoma. Pinda alikuwa kati ya wanachama 38 wa CCM waliojitosa katika kinyang’anyiro cha urais kwa tiketi ya chama hicho. Hata hivyo, jina lake lilikuwa miongoni mwa majina yaliyokatwa kwa mara ya kwanza na kubakia matano ambayo yalipelekwa kwenye Kamati Kuu (CC) ya CCM. Majina yaliyopelekwa kwenye kamati hiyo yalikuwa ni ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Said Salum na January Makamba. Majina hayo yalipelekwa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM ambapo wajumbe wake walipitisha majina matatu kati ya matano.
Waliopenya katika kinyang’anyito hicho ni Dk. Magufuli, Dk. Migiro na Amina na kupelekwa mbele ya Mkutano Mkuu na wajumbe kupiga kura na kumpata Dk. Magufuli atakayepeperusha bendera ya chama hicho kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pinda aliteuliwa kushika wadhifa wa Uwaziri Mkuu na Rais Jakaya Kikwete, baada ya aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Edward Lowassa, kujiuzulu baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond mwaka 2007.
|
Tuesday, July 21, 2015
PINDA AUTOSA RASMI UBUNGE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment