DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Friday, June 27, 2014

DK. SALIM ASEMA HANA MPANGO WA KUGOMBEA URAIS 2015

Waziri Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim (pichani) amesema hana mpango na hafikirii tena kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam jana, Dk Salim alisema alipowania nafasi hiyo mwaka 2005, hakuwa na ufahamu mzuri kuhusu mchakato huo lakini baadaye alibaini kwamba, mbali na rekodi ya utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang'anyiro hicho na kwamba hata watu wanaomfikiria na kutaja jina lake miongoni mwa wanaoweza kuwania tena nafasi hiyo, wanakosea.

"Sifikirii tena, hii ni zamu ya kizazi kingine. Ila nitaendelea kuisaidia nchi yangu katika nyanja mbalimbali kadri ya uwezo wangu," alisema.

Dk Salim ambaye mbali na uwaziri mkuu amewahi kushika nafasi nyingine mbalimbali kitaifa na kimataifa, alisema uzoefu alioupata katika kinyang'anyiro cha urais unatosha.

Alipoulizwa kama uzoefu huo ni mbaya au mzuri kwake, alisema ni mchanganyiko.

Dk Salim aliwahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na kushindwa kutokana na kura ya veto ya Marekani, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU). Pia aliwahi kuwa Rais wa Bunge Kuu la UN mwaka 1979 na 1980.

Licha ya kujitokeza mara moja kuomba uteuzi wa CCM kuwania urais 2005, nyota yake katika nafasi hiyo ilianza kuwaka tangu mwaka 1985 akiwa Waziri Mkuu pale aliposhindanishwa katika Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa pamoja aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi ambaye alipitishwa kiitifaki na kushinda kiti hicho.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisimulia jinsi Mwinyi alivyopita, kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais, hivyo wajumbe wa Kamati Kuu walikosa hoja na sababu za kumwacha na kumchukua Waziri Mkuu aliyekuwa chini yake kiitifaki.

"Makamu wa Rais ukimruka maana yake hatoshi, wakaona hawana maelezo hayo, ikabidi wamteue Mwinyi," alisema Msekwa.

Sifa za viongozi

Katika hatua nyingine, Dk Salim alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuandaa viongozi hasa mtu anayekwenda kushika nafasi ya urais atakayekwenda sambamba na mahitaji ya kizazi cha sasa alichokiita cha 'dot com'.

"Hapa sizungumzii viongozi wa CCM au wa Chadema au chama kingine, nazungumzia viongozi wa nchi watakaoweza kufanyia kazi matatizo ya Watanzania.

"Ni vizuri viongozi wakaandaliwa, isiwe mtu anaibuka tu anagawa hela halafu anashinda. Anatakiwa mtu atakayeweza kushughulikia matatizo hayo. Watanzania ni wapole na wavumilivu lakini wanazungumza. Hivyo anahitajika kiongozi atakayesikiliza mahitaji yao na kutoa suluhisho, si kutoa ahadi za uongo," alisema. Dk Salim alisema katika kipindi hiki, anahitajika kiongozi atakayekuwa juu ya tofauti za kisiasa, kidini, asili.

"Unajua hapa nchini kama ilivyo mahali pengine, ukiingiza mgawanyiko wa kidini wakati familia nyingi zina watu wa dini tofauti, wote wataathirika."

Viongozi na rushwa

Akizungumzia tatizo la rushwa, Dk Salim alisema ni kubwa na kadri linavyoongezeka, linakuwa adui wa uwajibikaji, demokrasia.

Alisema katika enzi za utumishi wake nje ya nchi, alikuwa akiona rushwa ilivyokithiri katika nchi mbalimbali, lakini hapa nyumbani pakiwa salama hadi akawa anasema Tanzania ina bahati, kauli ambayo hawezi kuisema sasa.

Dk Salim alibainisha kuwa uongozi unaoingia madarakani kwa rushwa hauwezi kuwa mzuri kwa nchi na athari zake zinaonekana hadi ngazi ya chini katika huduma za jamii kama mahakamani, polisi na hospitalini. (Picha na habari ni kwa hisani ya gazeti la Mwananchi)

No comments:

Post a Comment