DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Thursday, May 14, 2015

JK AMTEUA CP DIWANI ATHUMANI KUWA KAMISHNA MPYA WA MAKOSA YA JINAI TANZANIA (DCP)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Kamishna wa Polisi (CP) Diwani Athumani Msuya, kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (Director of Criminal Investigation).

Kabla ya uteuzi huu CP Msuya alikuwa Kaimu Kamishna wa kamisheni ya Intelijensia ya Jinai. CP Msuya anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Ndugu Robert S. Manumba ambaye amestaafu kwa mujibu wa Sheria.
Rais Kikwete pia amemteua Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Valentino Mlowola kuongoza Idara ya Intelijensia ya Jinai, kujaza nafasi inayoachwa na Kamishna Msuya.
Kabla ya Uteuzi huu, DCP Mlowola alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.Uteuzi huu umeanza tarehe 3 Mei, 2015
Imetolewa na; Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
12 Mei, 2015

MVUA YATIKISA JIJI LA DAR ES SAALAM!

Magari yakiwa yamenasa katika eneo la daraja Kitunda Relini, Kitunda jijini Dar es Salaam kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam na kujaza maji katika mito mingi jijini. Ni vyema madereva na watu wengine kuwa makini wanapoona maji mengi katika mito hiyo wasijaribu kuvuka kwani wanaweza kupata madhara kama hayo.

HIFADHI YA MLIMA KILIMANJARO YATANGAZA OFA YA KUPANDA MLIMA HUO KWA WATALII WA NDANI

Mhifadhi utalii katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Eva Mallya akizungumza juu ya ofa iliyotangazwa na hifadhi hiyo ya kupanda mlima huo kwa siku moja na kurudi hadi kilele cha Shira.
Afisa masoko wa KINAPA, Antypas Mgungusi akisistiza jambo wakati akizungumzia juu ya ofa ya safari ya kupanda Mlima Kilimanjaro huku akishauri wenye sherehe zao kutumia nafasi hiyo kupanda Mlima huo kwa ajili ya kufanya sherehe zao, alitaja sherehe ambazo zinaweza fanyika katika hifadhi hiyo ni pamoja na wale wenye kukumbuka siku zao za kuzaliwa wanaweza fanya hivyo wakiwa kileleni, lakini pia kwa wale wanaoenda Honey Moon baada ya ndoa pia wameshauriwa kufanya hivyo katika kipindi hiki cha ofa.

Ukiwa katika hifadhi hiyo utafurahia mandhari mbalimbali za mlima huo.

Wengine wanaweza pia kupanda na watoto wao.



Yapo mahema kwa ajili ya watalii wanaoendelea na safari.

Waliofanikiwa kufika kilele cha Shira hawakusita kuonesha furaha zao kwa kucheza .

JOHN GUIDO NYERERE AZIKWA JANA BUTIAMA

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma Mhashamu Michael Msonganzila akitoa heshima za mwisho kwa marehemu John Guido Nyerere baada ya kukamilika kwa ibada maalum iliyofanyika kwenye Kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Damu Azizi ya Yesu Jimbo la Musoma Parokia ya Butiama.
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye akizungumza na Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu Mstaafu Ndugu Edward Lowassa wakati wa mazishi ya John Guido Nyerere yaliyofanyika nyumbani kwa Baba wa Taifa ,Butiama.
Mama Maria Nyerere akiweka udongo kwenye kaburi la mtoto wake John Guido Nyerere.
Jeneza lenye mwili wa marehemu John Guido Nyerere likiteremshwa kaburini na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Asha-Rose Migiro akiweka udongo kwenye kaburi la John Guido Nyerere.
Mtoto wa mwisho wa marehemu John Guido Nyerere anayefahamika kwa jina la Wanzagi akilia kwa uchungu huku akifarijiwa na shangazi yake Anna Nyerere.
Ni huzuni kwa kila mtu.
 Mama Maria Nyerere akiweka shada la mau kwenye kaburi la mtoto wake John Guido Nyerere.
Mtoto wa Marehemu anayeishi Lusaka Zambia, Sofia Nyerere Mwape akiweka shada la maua kwenye kaburi la Baba yake marehemu John Nyerere.
 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akitoa heshima mbele ya kaburi la marehemu John Gaudo Nyerere mara baada ya kuweka taji la maua.
 Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki Shyrose Bhanji akiweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu John Nyerere kwenye mazishi yaliofanyika nyumbani kwa marehemu Baba wa Taifa Butiama.
Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakishiriki kuweka mashada ya maua kwenye kaburi la John Guido Nyerere.
Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Asha-Rose Migiro akisoma salaam za rambi rambi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wakati wa mazishi ya John Nyerere.
Emily Magige Nyerere akifafanua jambo wakati wa mazishi ya John Guido Nyerere. (Picha zote na Adam H. Mzee).

RAIS NKURUNZINZA WA BURUNDI NA JARIBIO LA KUPINDULIWA

Rais Jakaya Kiwete akiwa na Rais Piere Nkurunzinza wa Burundi jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa upatanishi. Marais wa EAC wameshauri kuahirishwa kwa uchaguzi wa Burundi uliokuwa ufanyike mwezi ujao.
Rais Piere Nkurunzinza wa Burundi.

Monday, May 11, 2015

JK ZIARANI NCHINI ALGERIA

Rais Jakaya Mrisho Kikwete na ujumbe wake akutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Algeria Mhe. Abdelaziz Bouteflika katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Algiers Jumapili May 10, 2015 katika siku ya pili ya ziara yake rasmi ya siku tatu nchini humo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiongea na waandishi wa habari baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Algeria katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Algiers Jumapili May 10, 2015 katika siku ya pili ya ziara yake rasmi ya siku tatu nchini humo.
7
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa ameongozana na Rais wa Baraza la Nchi ya Algeria Mhe. Abdulkhader Bensalah akiwasili katika ukumbi wa El-Mithak Residency jijini Algiers kwa dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Algeria Mhe. Abdelaziz Bouteflika katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Algiers Jumapili May 10, 2015 katika siku ya pili ya ziara yake rasmi ya siku tatu nchini humo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na mabalozi wa nchi za Kiafrika katika ukumbi wa El-Mithak Residency jijini Algiers baada ya dhifa ya kitaifa aliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Algeria Mhe. Abdelaziz Bouteflika katika Ikulu ya nchi hiyo jijini Algiers Jumapili May 10, 2015 katika siku ya pili ya ziara yake rasmi ya siku tatu nchini humo.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitambulishwa kwa viongozi mbalimbali na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Algeria Mhe. Abdelmalik Sellal katika kiunga cha Ikulu ya nchi hiyo cha Zeralda Jumapili Mei 10, 2015 katika siku ya pili ya ziara yake rasmi ya siku tatu nchini humo.

CHADEMA WAFANYA MKUTANO WAO JIJINI ARUSHA

Mheshimiwa Tundu Lissu akiwahutubia wakazi wa Arusha Mjini katika mkutano mkubwa ulioambatana na mvua kubwa hapo juzi.

Wakazi wa Arusha wakiwa katika mkutano mkubwa ulioambatana na mvua lakini walisema wasingeondoka hata kama mvua ya mawe ingenyesha.
Makamanda wakiwa wamelowa chapa chapa lakini bila kujali mvua wameweza kufanya mkutano kama kawaida.


TAASISI YA IMETOSHA IMETOA MSAADA KITUO CHA BUHANGIJA MKOANI SHINYANGA

Toka kushoto ni Kathrin Hoff, kijana Paulo, Masoud Kipanya na Balozi Henry Mdimu.

Taasisi ya Imetosha ya jijini Dar es Salaam leo hii imepeleka misaada mbali mbali katika kijiji cha watoto wasioona cha Buhangija, mkoani Shinyanga ambacho kwa sasa kinahifadhi pia watoto na vijana wenye ualbino takriban 300.
Misaada hiyo ikiwemo mabelo ya mitumba 2 moja la masweta na jingine la suruali za jeans, unga, mchele, maharage, sukari, chumvi, ndoo 3 za mafuta ya kupikia, sabuni za kufulia box 8, vile vile box 3 za vifaa vya hedhi vitakavyodumu miezi miwili pamoja na nguo za ndani dazeni 12 vyote hivo imegharimu Tsh milioni mbili na elfu sitini(2,060,000) ambazo zimetolewa na wanachama wa taasisi hiyo iliyojikita kupambana na mauaji ya watu wenye ualbino kwa njia ya elimu.
Akiongea na watoto na vijana hao Mwenyekiti Masoud Kipanya alisema taasisi hiyo inaangalia jinsi ya kutengeneza mazingira kwa kituo hicho kujijengea uwezo wa kujipatia chakula badala ya kutegemea wasamaria wema huja pale watakapojisikia wakati watoto katika kituo hicho wanahitaji kula kila siku.
Mkuu wa kituo hicho aliishukuru taasisi ya Imetosha kwa kuonesha mapenzi ya dhati na watoto wa kituo hicho na kuguswa na changamoto zinazowakuta, kwani si mara nyingi sana watu au taasisi kurudia kupeleka misaada kituoni hapo kitu ambacho Imetosha wamekifanya. Wiki 3 zilizopita taasisi hiyo ilipeleka msaada wa chakula kituoni hapo.
Awali mtafiti wa masuala yahusuyo watu wenye ualbino mJerumani Bi Kathrin Hoff alielezwa kufurahishwa na jitihada zinazooneshwa na Imetosha kwa uhamasishaji inayoufanya kwa jamii ya Ki Tanzania, pia amepongeza sana hatua ya Imetosha kutaka kukifanya kituo cha Buhangija kujitegemea badala ya kubaki tegemezi kama ilivyo sasa. Kathrin Hoff ni mhitimu toka chuo kikuu cha Mainz nchini Ujerumani.

UN WAMUUNGA MKONO JK KWA KAZI ZAKE

Rais Jakaya Kikwete 
JUMUIYA ya Kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini hapa, imeelezea msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila hali kazi na jukumu ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na Majanga Duniani linaloongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Jumuiya hiyo imeeleza msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa Kudumu wa nchi mbali mbali duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi iliyofanywa na Jopo hilo katika siku za mwanzo kabisa.
Jopo hilo lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon Aprili 2, mwaka huu, limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya duniani, na hasa magonjwa ya milipuko, kama ilivyokuwa ebola katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia bna Sierra Leone.

Baada ya wiki moja ya kazi kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo hilo kutoka Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, walikutana na Wawakilishi wa Kudumu wa mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea nini kimefanyika na nini kinatarajia kufanyika.
Baada ya maelezo ya wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN alisema kuwa Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo akisisitiza kuwa Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa kiasi cha dola za Marekani milioni moja (shilingi bilioni 1.9) kuunga mkono shughuli za Jopo hilo.
Mwakilishi wa Senegal alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.
Mwakilishi wa Ufaransa alisema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa moja na kuwa ni uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.
Mwakilishi wa Uingereza alipokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo, akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo kama ilivyoiunga mkono Sierra Leone wakati wa kukabiliana na ebola.
Mwakilishi wa Luxembourg alisema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu yake katika mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi.
Aidha, ameongeza kuwa nchi hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya (EU) itaongeza kazi yake katika kuchunguza athari za ebola na kiini chake. CHANZO: HABARI LEO