DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Thursday, October 31, 2013

SAKATA LA UDUKUZI: MAREKANI YAIGEUKA ULAYA


Wakuu wa ujasusi nchini Marekani 'wamewageuzia kibao' washirika wao wa Ulaya katika mgogoro unaohusu udukuzi wa mawasiliano ya simu, wakisema mashirika ya Ulaya ndiyo yaliyokusanya taarifa na kuzitoa kwa Marekani. 

Wakuu hao wa mashirika ya ujasusi ya Marekani waliyakanusha kuwa ni uongo, madai kwamba mashirika yao yalinasa mawasiliano ya mamilioni ya simu, na kusema magazeti ya Ulaya yaliyochapisha madai hayo, hayakuelewa data walizokuwa wanazitumia kutoa madai hayo.

Maelezo hayo yamekuja wakati afisa wa juu wa Marekani akisema Rais Barack Obama alikuwa akitafakari kuwapiga marufuku majasusi wa Marekani kunasa mawasiliano ya ya simu za viongozi wa mataifa washirika, kufuatia hasira za Ujerumani juu ya madai kwamba mawasiliano ya Kansela Angela Merkel yalidukuliwa.

Mkuu wa NSA, Jenerali Keith Alexander, na mkuruguenzi wa usalama wa taifa, James Clapper, walitoa ushahidi mbele ya bunge la Marekani na kusema kwamba msingi wa ripoti hizo ulikuwa kutolewa taarifa zilizokabidhiwa kwa magazeti ya Ulaya na Snowden.

"Madai ya waandishi wa habari wa gazeti la Le Monde la Ufaransa, El Mundo la Uhispania na L'Espresso la Italia kwamba NSA ilikusanya mamilioni ya taarifa za mawasiliano ya simu hazina ukweli wowote. Kwa kuweka mambo wazi kabisa, hizo siyo taarifa tulizozikusanya kuhusu raia wa Ulaya. Ni taarifa ambazo sisi pamoja na washirika wetu wa NATO tulizikusanya katika kuhakikisha usalama wa mataifa yetu na kusaidia operesheni zetu za kijeshi," alisema Jenerali.
Masaa machache kabla ya hapo, jarida la Wall Street liliripoti kwamba uchunguzi wa kielektroniki ulifanywa na mashirika ya kijasusi ya Ufaransa na Uhispania nje ya mipaka ya mataifa yao, na wakati mwingine katika uwanja wa vita na kutoa taarifa zao kwa NSA.

Ikiwa madai hayo yatakuwa kweli, yanaweza kuzifedhehesha serikali za mataifa ya Ulaya, ambazo zimeipinga kwa nguvu Marekani kwa madai ya kuwafanyia ujasusi raia wake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya bunge la Marekani, Dianne Feinstein, aliunga mkono utetezi wa wakuu hao wa ujasusi na kusema kuwa Marekani haikuzichunguza Ufaransa na Ujerumani, bali nchi hizo ndizo zilikuwa zinakusanya taarifa hizo, na kwamba Marekani ilikuwa inakusanya tu taarifa katika maeneo ya kivita ya NATO kama vile Afghanistan.

Hakukuwa na majibu ya mara moja kutoka kwa mashirika ya kijasusi ya mataifa ya Ulaya yaliyotajwa, lakini Alexanser na Clapper waliwambia wabunge kuwa mataifa ya kigeni pia yalikuwa yakiwafanyia ujasusi viongozi wa Marekani, na kufafanua kuwa kuwachunguza viongozi wa kigeni ndiyo msingi wa mchezo wa ujasusi kimataifa.

Wakati huo huo, maafisa wa ujasusi wa Ujerumani wanatarajiwa kukutana na wawakilishi wa mashirika ya ujasusi ya Marekani katika lkulu ya White House leo, kujadili madai ya ujasusi wa Marekani. Ujumbe wa Ujerumani unawahusisha mshauri wa sera ya kigeni wa Kansela Merkel na mratibu wa idara ya ujasusi ya Ujerumani.

Kwa upande wa Marekani, ujumbe wake unaowajumuisha mshauri mkuu wa usalama wa Rais Obama, Suzane Rice, mkurugenzi wa usalama wa taifa James Clapper na msaidizi wa rais wa usalama wa ndani na mapambano dhidi ya ugaidi, Lisa Monaco.

Rais Obama na Kansela Merkel walikubaliana katika mazungumzo mafupi kwa njia ya simu wiki iliyopita kuimarisha ushirikiano wa nchi zao katika masuala ya ujasusi, na msemaji wa NSA, Caitlin Hayden, alisema mkutano huu ni sehemu ya majadiliano hayo. (Habari ni kwa msaada wa Mashirika ya Habari ya Kimataifa)

Saturday, October 26, 2013

MAWASILIANO YA MERKEL YAKO SALAMA LICHA YA UDUKUZI

Serikali ya Ujerumani imesema mfumo wa mawasiliano wa Kansela Angela Merkel uko salama licha ya madai kuwa mashirika ya kijasusi ya Marekani yalidukua mawasilano yake ya simu yake ya mkononi.

Ufichuzi wa kuwa Shirika la Usalama la Taifa la Marekani (NSA) limekuwa likidukua mawasiliano ya raia wa bara la Ulaya na viongozi wake, limezorotesha uhusiano kati ya Marekani na washirika wake wa Ulaya.

Ujerumani na Brazil zinatarajiwa kuwasilisha azimio katika Umoja wa Mataifa pengine hata wiki ijayo la kutaka kupanuliwa kwa haki za kuwa na faragha katika mawasiliano ya mitandaoni na kumtaka Kamishna wa Kaki za Binadaamu wa umoja huo kulizingatia suala hilo.

Hapo jana gazeti moja la Uingereza liliripoti kuwa NSA ilidukua mawasiliano ya simu ya viongozi 35 kote duniani kundi la viongozi linalomjumuisha Merkel.Ujerumani itawatuma maafisa wake wakuu wa kijasusi kwenda katika Ikulu ya Marekani ya White House wiki ijayo, kutafuta majibu juu ya madai kwamba Marekani ilinasa mawasiliano ya simu ya mkononi ya Kansela Merkel. (Habari hii kwa hisani ya Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani)


UZINDUZI WA KAMPENI YA KITAIFA KWA NJIA YA VYOMBO VYA HABARI JUU YA KAZI ZENYE STAHA KWA WAFANYAKAZI WA MAJUMBANI

Chama cha wafanyakazi wa hifadhi, mahoteli, majumbani, huduma za jamii na ushauri (CHODAWU) kimeiomba serikali ya Tanzania kuridhia mkataba wa wafanyakazi wa majumbani wa kazi zenye staha namba 189  uliopitishwa kimataifa na shirika la kazi Duniani ILO mwaka 2011 ili uanze kutumika katika sheria zetu za nchi.
Mkataba huo wenye mapendekezo 201 umelenga zaidi kuhakikisha wafanyakazi wa majumbni wanapata haki zao za msingi katika sehemu za  kazi na mazingira mazuri ya kazi wanazofanya hii ikiwa ni pamoja na kujiunga katika vyama vya wafanyakazi, kupata mishahara iliyoidhinishwa kisheria, kupata mikataba ya ajira, kupata likizo za mwaka, uzazi na ugonjwa halikadhalika kujiunga na mifuko ya hifadhi za jamii.

Hayo yalisemwa leo hii na katibu wa CHODAWU Mkoa wa Dodoma Bi. Atupakisye Mtafya  alipokuwa akitoa taarifa ya CHODAWU wakati wa mkutano wa kuzindua kampeni ya kitaifa kwa njia ya vyombo vya habari juu ya kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa majumbani uliofanyika mjini Dodoma leo hii.

Akizungumzia kampeni hiyo inayofanywa kwa njia ya vyombo vya habari Bi. Atupakisye amesema kuwa lengo la kampeni ni kuipa jamii uelewa juu ya mkataba namba 189 wa kazi zenye staha kwa wafanyakazi majumbani, sheria za kazi na kusisitiza mazingira bora ya kazi. Amewataja wafanyakazi wa majumbani kama kundi kubwa ambapo kwa takwimu za ILO mwaka 2008 idadi ya wafanyakazi za majumbani ilikuwa milioni 5.2 na kusisitiza kuwa wanastahili haki kama wafanyakazi wengine.

Bi Atupakisye alibainisha kuwa wafanyakazi wa majumbani wanamchango mkubwa katika familia na uchumi wa nchi kwa kazi wanazofanya majumbani na pia kwa kuwapa fursa wafanyakazi wengine kufanya kazi za uzalishaji katika sekta rasmi na zisizo rasmi kwa ufanisi. Aliongeza kuwataka waajiri wazingatie viwango vya ajira vilivyoainishwa katika sheria ya ajira na mahusiano kazini pamoja na sheria ya taasisi za kazi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi wakati akizindua rasmi kampeni hiyo ya kuhamasisha kwa tumia vyombo vya habari aliwataka CHODAWU kuwa na mkakati wa kuanza na waajiri kwa kuwahamasisha watambue na kutekeleza haki za wafanyakazi majumbani kwani endapo wao hawatahamasika basi manyanyaso na uvunjifu wa haki ya wafanyakazi majumbani yataendelea kuwepo hata kama serikali itaridhia mkataba huo namba 189.

Dr. Nchimbi pia amewataka CHODAWU ktk kampeni yao ya kutaka serikali iridhie mkataba namba 189,wajaribu kuangalia na kutofautisha historia, mazingira,mikao ya kisera, ameelezea mkao wa mahoteli ni wa kiuchumi wakati wafanyakzi majumbani ni wakujikimu zaidi. Vilevile alisisitia tofauti za kutoa huduma muhimu kwa wafanyakazi ziangaliwe kwa kutoa mfano kuwa ni vigumu utoaji wa huduma kwa wafanyakazi ufanane kati ya familia ya watu kama walimu wa shule za msingi na mameneja au wakuu wa taasisi na mashirika/makampuni kwa kuwa hata vipato vyao havifanani.

Dr. Nchimbi mbali na kutambuaa umuhimu wa wafanyakazi wa majumbani kwa kazi zao wanazofanya majumbani pia ameonesha kutambua umuhimu mkubwa wa sekta ya ajira majumbani n kusema kuwa sekta ya ajira rasmi haina fursa nyingi kama sekta zisizo rasmi. Vilevile aliwaasa waajiri hususani wakinamama wenye tabia za kujisahau majumbani kuwaachia majukumu yote wafanyakazi wao nyumbani kuwa tabia hio imechangia kuvurug a familia zao kwani kumeibuka tatizo la waume zao kuanzisha mahusino ya kimapenzi/kiunyumba na wasaidizi majumbani.

Kwa upande wake mwakilishi wa ILO ambao ndio wafadhili wa kampeni ya kuhamasisha kazi zenye staha kwa wafanyakazi wa majumbaniaba kupitia vyombo vya habari Bi. Kokushubila Kabanza alijulisha kuwa wafanyakazi wa majumbani wamesahaulika sana na sheria zake za kazi hazitekelezwi hivyo kuitaka serikali nayo kuungana na nchi nyingine wanachama kuridhia mkataba namba 189 na kusema kuwa mpaka sas ni mataifa 10 tu wanachama ndio wameridhia Afrika Kusini na Moroko zikiwemo kw a upande w a Nchi za kiafrika na kuongeza kasi ya nchi wanachama kuridhia bado ni ndogo sana.

Wednesday, October 23, 2013

TAARIFA KWA UMMA



MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA MJINI DODOMA
(DUWASA)

TAARIFA KUTOKA DUWASA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma imekuwa ikiathirika katika uzalishaji na usambazaji majisafi kwa wateja wake kutokana na makatizo ya umeme wa TANESCO ya mara kwa mara jambo ambalo limekuwa likisababisha usumbufu kwa wateja kwa kukosa huduma muhimu ya maji.
Kwa takwimu, katika kipindi cha mwezi Oktoba 2008 hadi mwezi Oktoba 2013 DUWASA haikuzalisha, kusukuma na kusambaza majisafi kwa wateja wake kwa jumla ya saa 1,548 kutokana na Makatizo ya umeme wa TANESCO kwenye visima na mitambo ya kuzalisha na kusukumia majisafi ambao ulikatika kwa jumla ya saa 1,548. Makatizo hayo ya umeme kuanzia mwezi Oktoba 2008 hadi Oktoba 2013 yamesababisha DUWASA kutozalisha majisafi kiasi cha mita za ujazo 2,012,400 sawa na lita 2,012,400,000 (lita bilioni mbili kumi na mbili milioni na mia nne elfu).
Maeneo mengi ya mji yamekuwa yakiathirika na upatikanaji wa majisafi kufuatia makatizo hayo ya umeme.


Eng. Peter A. Mokiwa
MKURUGENZI MTENDAJI
DUWASA