DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Thursday, March 10, 2016

SERIKALI IMEDHAMIRIA KUUNDA MAMLAKA KUU YA MAPATO YA TAIFA

Kaimu Kamishna wa TRA Alphayo Kidata akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika mkutano wa kutoa taarifa juu ya ukusanyaji wa kodi kwa mwezi Februari, 2016.
Serikali ipo kwenye mpango wa kuunda Mamlaka ya Mapato Kuu ya Taifa nje ya Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) iliyopo kwa sasa ili kuondokana na malalamiko ya kero za kodi kwa wananchi wenye kipato cha chini.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Alphayo Kidata alipokuwa akifafanua kuhusu juhudi za Serikali katika kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kuweza kumudu kulipa kiwango cha kodi kinachowekwa na na Mamlaka hiyo.
“ Napenda kuwaambia umma wa watanzania kwamba Serikali ya Awamu ya tano inawajali watu wake na ndio maana imeona kuwa kuna haja ya kuunda Mamlaka moja ya utozaji wa kodi itakayojumuisha taasisi zote zinazohusika na kukusanya mapato nje ya kodi na ushuru ili kuondokana na malalamiko mengi ya wananchi juu ya utozaji wa kodi hasa katika Halmashauri zetu”Alisema Kidata.
“Kamishna Kidata amesema kuwa katika dunia hii hakuna Serikali ambayo imechaguliwa na wananchi ikaamua tu kuwakandamiza wananchi wake katika jambo lolote lile hivyo basi kwa sasaserikali ipo katika mchakato wa kuunda Mamlaka hiyo ambayo itasaidia kuweka viwango vya kodi ambavyo wananchi wa hali ya chini watamudu kulipa kutokana na biashara au kazi wanazozifanya.
Kamishna huyo ameongeza kuwa Mamlaka yake kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazokusanya kodi katika Halmashauri nchini watahakikisha wanalipatia ufumbuzi suala la kero ya kodi kwa wananchi wa hali ya chini kwa kupata muafaka ambao utasaidia pande zote mbili bila kukandamiza upande wowote iwe Serikali ama mwananchi wa kawaida.
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuwa na rekodi nzuri ya ukusanyaji wa kodi ila kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu kodi ambazo zimekuwa kero na hazina tija. Hivyo Serikali imejipanga kuiongezea nguvu Mamlaka hiyo kwa kuipa uwezo wa kukusanya na mapato ambayo hayatokani na kodi toka katika wizara, mashirika,tasisi za serikalina Halmashauri zote nchini.



No comments:

Post a Comment