Serikali imekunjua makucha yake katika kudhibiti
ada zinazotozwa katika vyombo vya utoaji elimu chini.
Jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.
Shukuru Kawambwa alizindua rasmi mfumo mpya wa ulipaji ada katika vyuo vya
elimu ya juu, huku akisema utasaidia kudhibiti viwango vya ada vinavyotozwa kwa
wanafunzi.
Akizindua mfumo huo jijini Dar es Salaam, Dk.
Kawambwa alisema Serikali imeanzisha mfumo huo unaotarajiwa kuanza kutumika
mwaka huu katika vyuo vyote, kwa lengo la kudhibiti ada kulingana na fani
zinazotolewa.
"Sasa natarajia nitapata usingizi wa
kueleweka maana kelele za viwango vya ada zilikuwa ni kubwa, kila chuo kilikuwa
na ada yake. Niliulizwa vigezo vinavyotumika kupanga sikuwa na jibu, lakini
sasa nitakuwa na majibu tena yanayoeleweka," alisema.
Suala la viwango vya ada katika shule na vyuo
binafsi liliwahi kuzungumziwa kwa kina siku za nyuma, huku Rais Jakaya Kikwete
na Waziri Kawambwa wakinukuliwa kwa nyakati tofauti kutaka taasisi za elimu
kupunguza viwango vya elimu. Aprili 2013 akifungua Mkutano Mkuu Maalumu wa
Chama cha Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyokuwa vya Serikali
(Tamongsco) uliofanyika mkoani Mbeya, Rais Kikwete alisema: "Elimu ni
huduma muhimu na haki kwa mtoto. Siyo vyema kugeuzwa kuwa biashara ya kuleta
faida kubwa.''
Aliongeza kuwa Serikali ilikuwa katika mchakato
wa kutathmini ada zinazotozwa vyuoni na sekondari ili kupendekeza viwango
halisi vinavyopaswa kutozwa.
Kwa sasa udadisi wa gazeti hili umebaini kuwa
wanafunzi walioanza masomo katika mwaka wa fedha 2013/2014 wanatozwa ada
kuanzia Sh360,000 kwa mwaka hadi Sh9,900,000.
Kwa mujibu wa Dk. Kawambwa, mfumo huu ambao
baadaye utaendelea hadi shule za sekondari na msingi, umepatikana kupitia
kikosi kazi cha wataalamu ambacho pamoja na majukumu mengine kilipewa kazi ya
kutathmini gharama.
Dk. Kawambwa alisema moja ya faida ya utaratibu
huo mpya ni kudhibiti taasisi zinazotoza ada kubwa kwa sababu za binafsi
ikiwamo biashara.
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini
Makumira cha Dar es Salaam (Tudarco), Profesa Uswege Minga alisema endapo
gharama hizo zitakuwa sawa, vyuo binafsi vitaathirika kwa sababu ni gharama
kubwa kuendesha chuo kikuu. (Habari kwa hisani ya MjengwaBlog).
|
No comments:
Post a Comment