Katika siku za karibuni, kumekuwepo
na habari nyingi, baadhi zenye kuchanganya umma na nyingine hata zikidai kuwa
baadhi ya wafanyakazi nchini wanapanga kuandamana endapo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete atakubaliana na maombi
ya nyongeza ya posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba .
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu (DPC), inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu habari hizo kama ifuatavyo:
(a) Kwamba Mhe.
Rais hajapata kupokea maombi yoyote kutoka kwa Uongozi wa Bunge ya kumwomba
aridhie kuongezwa kwa posho ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kiwango
cha sasa cha sh. 300,000 (laki tatu)kwa siku hadi kufikia sh. 500,000 (laki
tano) ama sh. 700,000 (laki saba) kama ambavyo imekuwa ikivumishwa katika
baadhi ya vyombo vya habari.
(b) Na kwamba kwa
sababu Mhe. Rais hajapata kupokea maombi ya nyongeza ya posho hiyo, hakuna
ongezeko lolote la posho ambalo Mhe. Rais ameliidhinisha.
(c) Kwamba
alichopokea Mhe. Rais ni maombi ya Uongozi wa Bunge wa kuomba Mhe. Rais aridhie
kufanyika marekebisho katika kiwango cha malipo ya siku kwa Wajumbe hao cha sh.
300,000 (laki tatu) ili posho ya kikao iwe posho ya kujikimu na posho ya
kujikimu iwe ndio posho ya kikao.
(d) Kwamba Mhe.
Rais amelikubali ombi hilo la Uongozi wa Bunge la kufanyika kwa marekebisho
katika mpangilio huo wa posho lakini kiwango cha malipo ya kila siku ya Wajumbe
hao kibakie kile kile cha sh. 300,000 (laki tatu) kwa siku.
(e) Kwamba tayari
Mhe. Rais amekwishaujulisha Uongozi wa Bunge kuhusu uamuzi wake huo wa kukubali
yafanyike marekebisho lakini kiwango kibakie kile kile cha sh. 300,000 (laki
tatu) kwa siku.
(f) Hivyo, Mhe.
Rais hajaongeza kiwango cha malipo ya Wajumbe hao kwa sababu hakupata kuombwa
wakati wowote kuongeza kiasi hicho.
Ni matarajio ya Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais, Ikulu, kuwa maelezo haya ya ufafanuzi yatasaidia kufunga
mjadala ambalo msingi wake kwa kweli umekuwa haupo.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
No comments:
Post a Comment