Kiingilio
cha chini kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Simba
itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni
sh. 7,000.
Washabiki
watakaolipa kiingilio hicho ni wale watakaokaa viti vya rangi ya bluu na kijani
ambavyo jumla yake ni 36,693 katika uwanja huo wenye viti 57,558. Viingilio
vingine ni sh. 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 20,000 kwa VIP B na C
wakati VIP A itakuwa sh. 30,000.
Tiketi
zitakazotumika kwenye mechi hiyo ni za elektroniki, na zimeanza kuuzwa jana (Oktoba
13 mwaka huu). Tiketi zinapatikana kwa mtandao wa M-PESA, CRDB Simbanking na
maduka ya CRDB Fahari Huduma ambayo yapo zaidi ya mia moja sehemu mbalimbali
jijini Dar es Salaam.
Mechi
hiyo namba 27 itakayochezeshwa na mwamuzi Israel Mujuni Nkongo akisaidiwa na
John Kanyenye na Ferdinand Chacha itaanza saa 10 kamili jioni. Kamishna wa
mechi hiyo ni Salum Kikwamba kutoka mkoani Kilimanjaro.
Washabiki
wanatakiwa kununua tiketi mapema, kwani hazitauzwa uwanjani siku ya mechi.
Milango yote ukiwemo ule wa upande wa Mbagala (Uwanja wa Ndani) itafunguliwa kwa
ajili ya washabiki, na itakuwa wazi kuanzia saa 4 asubuhi.
Magari
maalumu tu yenye stika ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia uwanjani kwa kupitia
Barabara ya Mandela. Pia washabiki hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakiwa na
silaha, vitu vya vyuma na mabegi makubwa. Barabara ya kuingilia upande wa Chang’ombe
itafungwa kwa watumiaji wa magari.
|