Serikali
ya Uganda inawashutumu baadhi ya maafisa wa Umoja wa Ulaya kwa kile
inachosema wanaingilia mambo ya ndani, huku ikimtia nguvuni Jenerali
David Sejusa kwa tuhuma za kujihusisha na siasa akiwa mwanajeshi.
Kundi la
wangalizi 30 wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya lilianza shughuli wiki
tatu zilizopita likifuatilia jinsi kampeni zinavyoendeshwa, kushauriana
na wadau wa uchaguzi huo wakiwemo wagombea wa upinzani na pia vyombo vya
usalama na Tume ya Uchaguzi, lakini msemaji wa serikali ya Uganda,
Ofwono Opondo, amewaambia wanahabari kwamba serikali imegundua njama za
baadhi ya waangalizi hao kushirikiana na maafisa wa Umoja wa Ulaya
kupendelea upinzani.
Opondo alisema waangalizi hao wanafadhili "uanzishaji wa kituo kisicho rasmi cha kukusanyia na kuchuja matokeo ya uchaguzi."
Madai
haya ya serikali yanayoibuka siku 17 tu kabla ya uchaguzi kufanyika,
yanapelekea kuwepo kwa mazingira ya ukosefu wa imani miongoni mwa wadau
mbalimbali kama suala zima la uchaguzi pamoja na matokeo ya zoezi hilo
kuwa ya haki na huru.
Jenerali Sejusa akamatwa
Wakati
huo huo, kitendo cha kumkamata aliyekuwa wakati mmoja mkuu wa vyombo vya
ujasusi vya Uganda, Jenerali David Sejusa, kiliwashangaza wengi.
Jenerali Sejusa, ambaye ni mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Kaguta
Museveni, alikamatwa hapo jana na kuzuiliwa katika kambi ya kijeshi ya
Makindye nje kidogo ya jiji la Kampala.
Wakili wa jenerali huyo, David Mugisha, alisema mteja wake "hakuruhusiwa kushauriana na yeyote mkiwemo mawakili wake."
Huku
mawakili hao wakielezea kutofahamu hasa sababu za kukamatwa kwa jenerali
huyo ambaye amekuwa akiandamana na Dk. Kizza Besigye katika kampeni
zake, msemaji wa serikali, Opondo, amefahamisha kwamba ni kuhusiana na
shughuli zake za kisiasa, "ikiwemo kubuni makundi ya watu kumi kumi
kusababisha vurugu kabla, wakati na baada ya uchaguzi."
Duru ya
mwisho ya kampeni za wagombea urais watatu, Rais Museveni, Dk. Besigye
na Amama Mbabazi, itakuwa jijini Kampala, huku serikali ikisema itafanya
kila iwezalo kuhakikisha kampeni hizo zinafanyika katika mazingira ya
amani na utulivu na kwamba itakabiliana na jaribio lolote la kusababisha
vurugu.
|
No comments:
Post a Comment