WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu,
ameendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi wa kudumu kuhusiana na
changamoto zinazowakumba wadau wa biashara ya utalii nchini. Katika kuhakikisha hilo linafanyika kwa mafanikio na kwa
haraka, Nyalandu ametangaza kuanza kwa vikao vitakavyowakutanisha
wataalamu wa Wizara zinazohusika na maliasili na utalii za Tanzania na
Kenya kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali iili yapatiwe
ufumbuzi kwa maslahi ya pande zote. Hatua hiyo
imetokana na hivi karibuni Serikali ya Kenya kuyazuia magari ya utalii
kutoka Tanzania kuingiza watalii kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Jomo Kenyatta, hivyo kusababisha usumbufu
mkubwa. Hata hivyo, Nyalandu aliingilia kati kwa
kuzungumza na Waziri wa Utalii wa Kenya, Phillys Kandie na kufikiwa
kwa makubaliano ya kuruhusiwa na hapo wazo wa wizara hizo kukutana
likaibuliwa. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake jana, Nyalandu alisema vikao ya wataalamu hao vitaanza rasmi
Februari 3, mwaka huu, jijini Arusha ambapo vitahusisha pia wataalamu
kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.Alisema
vikao hivyo vitajadili masuala mbalimbali ili kuhakikisha changamoto
zote zinawaikabili sekta ya utalii kwa nchi hizo mbili zinapatiwa
ufumbuzi. Aliongeza kuwa hatua hiyo pia inalenga
kuimarisha ushirikiano pamoja na kuongeza ulinzi kwenye mbuga za
wanyama na mapori ya akiba dhidi ya mtandao wa ujangili. Hata hivyo, aliweka wazi kuwa hoja kuhusiana na mpaka wa
Borongoja haitajadiliwa kwenye vikao hivyo kwa kuwa si sehemu ya
ajenda. “Nchi zetu hizi zinategemeana sana katika
biashara ya utalii hivyo, kuna makubaliano tuliyafikia muda mrefu huko
nyuma lakini yanaonekana kuanza kuwa na changamoto hivyo ni lazima
tujadili ili tuweze kusonga mbele. Hatutaki watalii wanaokuja kupumzika
wasumbuke kwani itakuwa ni hasara kwa wafanyabiashara wetu na
kutahatarisha uchumi wa taifa…daima lazima tusonge mbele,” alisema
Nyalandu. Aliongeza kuwa baada ya mkutano wa
wataalamu utafuatiwa na wa makatibu wakuu wa wizara hizo
utakaofanyika Februari 4 mwaka huu kisha utahitimishwa na wa
mawaziri utakaofanyika Februari 5. Nyalandu alisema ana
imani mikutano hiyo itatoka na mwanga mpya na maboresho kwa sekta
ya utalii na kusisitiza maslahi ya pande zote yatazingatiwa.
Alisema kuwa nia ya Tanzania ni kuendeleza Jumuia ya Afrika
Mashariki na mahusiano yake mazuri na si kugombana na kuharibu
uhusiano huo.Alisema daima Tanzania itakuwa makini
kuhakikisha mahusiano yanakaa sawa katika majadiliano hayo na
kwamba kusije kutokea jambo likaleta madhara kwa watu wengine. Nyalandu aliongeza Tanzania itafanya biashara za utalii na
watu wengine kuhakikisha wanaendelea kulinda rasilimali za taifa
sambamba na wafanyabiashara wakubwa wa kitalii na
wadogo. | | |
No comments:
Post a Comment