WASANII wa muziki wa kizazi kipya, jana walitoa burudani ya
aina yake pamoja na elimu kwa vijana juu ya ushiriki wao katika masuala ya nchi
kwenye viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam. Wakiongowa na Hamis
Mwinjuma ‘Mwana FA’ pamoja na Niki wa Pili, wasanii zaidi ya 10 waliwapagawisha
mamia ya mashabiki waliojitokeza kwenye viwanja hivyo kupata elimu
hiyo kwa njia ya burudani.
Akizungumza kabla ya kuimba
nyimbo zake kali, Mwana FA akitumia tamasha hilo lililopewa jina la ‘Tuonane Januari’,
aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu na
kuchagua viongozi wanaowataka. “Vijana wenzangu..., tusisubiri
watu wengine watufanyie maamuzi.., ni sisi wenyewe tunatakiwa kuamua
tunachokitaka, tushiriki kwenye masuala nyeti ya nchi..., kuna uchaguzi mkuu
unakuja, vijana tuwe mstari wa mbele na tuchague viongozi tunaowataka,” alisema
Mwana FA. Mara baada ya kusema hayo,
alianza kuimba nyimbo zake zinazobamba kwa sasa ukiwemo, mfalme ambao
uliwapagawisha mashabiki waliofurika uwanjani hapo. Mbali na Mwana FA, pia Niki wa
pili alipata mapokezi makubwa uwanjani hapo kwa nyimbo zake kali huku pia
akisisitiza vijana kuchukua maamuzi sasa ya kuchagua viongozi wanaowataka.
Wanamuziki
wengine waliokonga nyoyo za mashabiki hao ni
pamoja na Shilole (Shishi Baby), Fid Q, Ditto, Linah, Navy and Kenzo, Dogo Janja,
Madee, Chegge, Temba, Mwasiti na Stamina, ambao nyimbo zao ziliwafanya
mashabiki
waliojitokeza kuimba nao pamoja. Tamasha hilo pia lilifanyika katika mikoa ya Njombe na
Morogoro ambapo linalengo la kutoa elimu kwa vijana juu ya kuwa karibu na
kushiriki matukio muhimu ya nchi hususan uchaguzi mkuu wa rais na wabunge ambao utafanyika
Oktoba mwaka huu. Pichani juu Mkali wa muziki wa kizazi kipya Mwana FA akitumbuiza katika
tamasha la Tuo8January lililofanyika katika viwanja vya MwembeYanga juzi.
|
No comments:
Post a Comment