DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Tuesday, September 01, 2015

WAGOMBEA UBUNGE 38 WALIOWEKEWA PINGAMIZI KUENDELEA NA KAMPENI

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damiani Lubuva.

Na Anitha Jonas – MAELEZO.TUME ya Taifa ya Uchaguzi  nchini  imefuta rufaa 38 za wagombea nafasi za ubunge kati ya 54 zilizowasilishwa kupinga baadhi ya wagombea hao kwa kuwatuhumu kutotimiza vigezo mbalimbali na kusema wagombea hao wanaweza kuendelea na Kampeni majimboni mwao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Uchaguzi  Bw. Kailima Ramadhan kwenye mkutano na waandishi wa habari.Alisema kuwa baada ya Wakurugenzi wanaoshughulikia uchaguzi kuzipitia, waligundua kuwa rufaa hizo waliziona hazina mantiki na kukosa ushahidi wa kutosha.
“Wagombea waliokuwa wamewekewa pingamizi na kuenguliwa katika uchaguzi ni 16 na Tume imewarudisha wagombea 13 kati ya hao na waliobaki watatu, Tume imeridhia maamuzi ya wasimamizi wa Uchaguzi”, alisema Bw. Ramadhani.
Aliongeza kuwa Tume hiyo inaendelea kupitia rufaa za wabunge zilizobaki  kwa kushirikiana na wasimamizi wa uchaguzi  ili kupata vielelezo  vinavyohusika na pindi itakapokamilisha zoezi hilo itatoa  taarifa yake ikiwa ni pamoja na rufaa 198 za madiwani kutoka Halimashauri mbalimbali nchini.
Aidha  alisema kuwa Tume hiyo  itaendelea kusimamia haki na kufanya maamuzi ya kuzingatia sheria kwa wagombea wa vyama vyote vilivyoshiriki katika uchaguzi wa mwaka huu na kuwataka kuwa na imani na kazi inayofanywa na Tume katika rufaa hizo.
Mbali na hayo Mkurugenzi  wa uchaguzi alisema kuwa  Tume inatarajia kuanza zoezi la uhakiki wa daftari la mpiga kura visiwani Zanzibar kuanzia tarehe kesho kutwa (03/09/2015) ambapo zoezi hilo litadumu kwa muda wa siku saba.
Akiongelea juu ya uhakiki wa taarifa za mpiga kura  aliyejiandikisha alisema unaweza kuhakiki taarifa zako kwa kupitia mtandao wa tume www.nec.go.tz au kwa  kupiga *152*00// katika simu na kupata taarifa zote.

No comments:

Post a Comment