Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika limekubaliana kutuma
kikosi cha wanajeshi 5,000 wa kuweka amani nchini Burundi, baada ya
mkutano wa nchi 54 kuonya kuwa hawatoruhusu mauwaji ya halaiki
kufanyika.
Mwana diplomasia mmoja amesema Baraza hilo linachukua hatua hii kwa mara
ya kwanza kwa kutekeleza sheria ambayo inaruhusu kutuma kikosi cha
wanajeshi bila idhini ya nchi husika. Burundi ambayo maafisa wa Umoja wa
Mataifa wamesema inaelekea kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa
wenyewe,imesema hakuna haja ya kutuma kikosi cha kulinda amani nchini
humo.
Uamuzi wa Umoja wa Afrika ambao ulifikiwa hapo jana jioni,unahitaji
kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,ambalo limekuwa
likitafakari namna ya kuusuluhisha mzozo wa Burundi ikiwemo kutuma
kikosi cha kulinda amani.
Afisa mkuu wa Umoja wa Afrika Bonaventure Cakpo Guebegde ameliambia
shirika la habari la AFP kuwa wanajeshi hao watakuwa chini ya kikosi cha
dharura cha Afrika Mashariki. Naye mwana diplomasia wa mojawapo ya nchi
wanachama wa baraza hilo la amani na usalama la Umoja wa Afrika
ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wamekubaliana kutumwa kwa
kikosi cha wanajeshi 5000 ambapo mojawapo ya majukumu yao itakuwa
kuwalinda raia.
Hofu ya kuongezeka kwa vurugu
Maafisa wa Umoja wa Mataifa na mabalozi wa mataifa ya magharibi
wameelezea hofu yao juu ya kuongezeka kwa vurugu nchini Burundi nchi
ambayo imetoka kwenye mapigano ya kikabila yaliyozuka mwaka 2005 baada
ya nchi hiyo kushuhudia miaka 12 ya vita.
Umoja wa Mataifa umesema watu wasiopungua 400 wameuawa tangu mwezi
Aprili wakati mzozo ulipozuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusema
anawania muhula wa tatu uongozini.Mzozo huo unahusisha wapinzani
waliopinga kuchaguliwa tena kwa Rais huyo na wanaomuunga mkono.
Mapigano hayo yamefanya kanda hiyo kuwa katika hali tete miongo kadhaa
baada ya mauaji ya halaiki katika nchi jirani ya Rwanda.Vita hivyo
vimetokea zaidi katika mji mkuu Bujumbura,ambapo wavamizi walivamia
kambi za kijeshi siku ya Ijumaa. Karibu watu 90 waliuwawa kwenye ghasia
hizo.
Orodha ya watakaowekewa vikwazo kuwasilishwa
Wanadiplomasia wanahofia mapigano hayo huenda yakazua migawanyiko ya
kikabila.Mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yamehusisha jeshi ambalo
wakati huo liliongozwa na kabila la watu wachache la Watusti dhidi ya
makundi ya waasi ya kabila la wahutu walio wengi likiwemo moja
linaloongozwa na Nkurunziza.
Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika limemtaka mwenyekiti wa
Tume ya Umoja huo Nkosazana Dlamini Zuma,kuwasilisha katika muda wa wiki
moja orodha ya watu watakaowekewa vikwazo.
Rais wa Burundi alisema hapo jana nchi yake iko tayari kufanya
mazungumzo .Wapinzani hata hivyo wamepuuza matamshi hayo hapo awali
wakisema serikali haijajitolea kujadili maswala muhimu ikiwemo hilo la
awamu mpya ya Rais Nkurunziza.
Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters/AFP
Mwandishi:Yusuf Saumu
|
No comments:
Post a Comment