JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425 |
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, amemtumia
salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu
Tarcisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu Mstaafu Plasdus Gervas
Nkalanga (OSB) kilichotokea Ijumaa tarehe 18 Desemba, 2015 katika
hospitali ya Mtakatifu Joseph Peramiho, Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.
Mhashamu
Askofu Nkalanga aliyekua Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba alistaafu
uaskofu mwaka 1974 na kujiunga na watawa wabenediktini wamonaki ambapo
aliamua kwenda kuishi katika Abasia ya Hanga iliyopo katika Wilaya ya
Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Katika
salamu zake Rais Magufuli amesema Askofu Nkalanga aliyefariki dunia
akiwa na umri wa miaka 96 atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa
kuhimiza imani na uchapakazi kazi katika kipindi chote cha miaka 54 ya
uaskofu wake na utawa wake akiwa katika Abasia ya Hanga.
Amesema Marehemu Askofu Nkalanga ambaye baada ya kustaafu aliamua kuingia katika utawa akianzia katika ngazi ya chini kabisa ya Unovisi hadi
alipofunga nadhili za milele za utawa mwaka 2009, ameacha mfano mzuri
unaohimiza jamii kuishi kwa upendo, unyenyekevu na kutokata tamaa.
"Kupitia
kwako Baba Askofu Ngalalekumtwa napenda kuwapa pole nyingi Askofu Mkuu
wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea, Abate wa Abasia ya Hanga, watawa na
waumini wote wa kanisa Katoliki kwa kupoteza mtu muhimu aliyetoa mchango
mkubwa katika maendeleo ya kanisa na jamii kwa ujumla" amesema Rais
Magufuli.
Rais
John Pombe Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho ya
Marehemu Mhashamu Askofu Mstaafu Plasdus Gervas Nkalanga mahali pema
peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
20 Desemba, 2015
No comments:
Post a Comment