DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Monday, December 21, 2015

WANYARWANDA WAUNGA MKONO MABADILIKO YA KATIBA

Rais Paul Kagame akipiga kura
Wanyarwanda wamepiga kura kwa kauli moja kubadilisha katiba kumruhusu rais Paul Kagame kuitawala nchi hiyo hadi mwaka 2034.
Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa tume ya uchaguzi jana Jumamosi(19.12.2015) kutokana na kura ya maoni iliyofanyika nchini humo.
Kura ya "Ndio" ikikubali mabadiliko ya katiba imepata asilimia 98.4, na asilimia 1.6 tu ya wapiga kura ndio waliopinga, kwa mujibu wa hesabu za mwisho za kura hiyo ya maoni iliyotolewa siku ya Jumamosi kutoka katika wilaya zote 30 za uchaguzi nchini humo pamoja na kura zilizopigwa nje ya nchi.
Tume ya uchaguzi hata hivyo imesema matokeo hayo bado ni ya awali.
Karani katika kituo cha uchaguzi akikabidhi karatasi ya kura.
"Tumeona matakwa ya wananchi. Ni wazi kwa kile wananchi wanachotaka , wanachotaka kufanikisha," amesema mkuu wa tume ya uchaguzi ya taifa Kalisa Mbanda.
Kagame sasa anaweza kutawala kwa miaka 17 mingine
Kagame , mwenye umri wa miaka 58, sasa anaweza kuwa madarakani kwa miaka mingine 17 ijayo.
"Kile kinachotokea ni chaguo la wananchi ," amewaambia waandishi habari baada ya kupiga kura yake siku ya Ijumaa.
Mabadiliko hayo yanamruhusu Kagame kugombea muhula wa tatu wa kipindi cha miaka saba ya uongozi mwaka 2017, ambapo sheria hizo mpya zitaanza kutumika na ataweza kugombea tena kwa vipindi vingine viwili vya miaka mitano.
Marekani na Umoja wa Ulaya wameshutumu mapendekezo hayo ya mabadiliko ya katiba kwamba yanakandamiza demokrasi katika taifa hilo la Afrika ya kati, wakati ikulu ya Marekani ya White House , jana Jumamosi ilimtaka Kagame kuheshimu muda wa mwisho wa kipindi chake cha uongozi.
"Marekani imekatishwa tamaa kwamba kura ya maoni imeitishwa katika kipindi kifupi kubadilisha katiba ya Rwanda na kuanzisha vipengee vya muda wa mwisho wa uongozi," taarifa hiyo imesema.
"Rais Kagame , ambaye kwa njia nyingi ameiimarisha na kuiendeleza Rwanda, sasa ana fursa ya kihistoria kuweka heba ya urithi wake kwa kuchukua hatua ya kuheshimu kile anachopaswa kukitenda kwa kuheshimu muda wake wa mwisho madarakani uliowekwa wakati akiingia madarakani," taarifa hiyo imeongeza.
Siku ya Ijumaa (18.12.2015), ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Kigali umesema kumekuwa na ukosefu wa "muda wa kutosha na nafasi kwa ajili ya mjadala" juu ya suala hilo, ambapo tarehe ya kura ya maoni ilitangazwa Desemba 8 na mswada wa mabadiliko " ulichapishwa tu chini ya siku moja kabla ya kura kufanyika."
" Muda mfupi kati ya kutangazwa na kufanyika kwa kura ya maoni kumesababisha kutokuwa na nafasi kwa vyama vyote kuwasilisha mawazo yao," Umoja wa ulaya umesema.
Kagame ameiongoza Rwanda tangu jeshi lake la waasi linaoundwa na Watutsi, Rwandan Patriotic Front (RPF), kumaliza mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyofanywa na Wahutu wenye msimamo mkali ambao ndio wengi nchini humo, wakati watu wanaokadiriwa kufikia laki nane waliuwawa, wengi wao wakiwa Watutsi.
Afrika ina watawala wanaong'ang'ania madaraka
Suala la watalawa wanaong'ang'ania madarakani kwa muda mrefu limesababisha ghasia katika bara la Afrika, ambako baadhi ya watalawa wamekuwa madarakani kwa miongo kadhaa, na Kagame sio wa kwanza katika miaka ya hivi karibuni kujaribu kubadilisha katiba ili kubakia madarakani.
Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza alishinda kipindi cha tatu cha uongozi ambacho kilishutumiwa duniani mapema mwaka huu, baada ya mzozo wa kikatiba na juhudi zake za kutaka kuchaguliwa tena ambazo zilizusha jaribio lililoshindwa la mapinduzi na kusababisha miezi kadhaa ya vurugu.
Katika jamhuri ya Congo, serikali ya rais Denis Sassou Nguesso mwezi Oktoba ilidai kupata ushindi wa kishondo katika kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba ambayo yanamfanya rais huyo kupata uhalali wa kurefusha kipindi chake cha uongozi uliodumu kwa miongo mitatu madarakani.
Na mwaka uliopita , mtawala aliyetawala kwa mkono wa chuma nchini Burkina Faso, Blaise Compaore, aliangushwa na maandamano ya umma baada ya kujaribu kurefusha utawala wake wa miaka 27.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Isaac gamba
Chanzo:DW


No comments:

Post a Comment