Mtawa
wa Kanisa Katoliki Parokia ya Chang'ombe jijini Dar es Salaam, Dafrosa
Clement akiwapaka majivu waamini wa Kikristo wa kanisa hilo juzi ikiwa
ni ishara ya kuanza safari ya kiroho ya mfungo na majuto kwa ajili ya
maandalizi ya Pasaka lakini zaidi sana kwa ajili ya
maandalizi ya maisha ya utakatifu milele.
***********
Baba
Mtakatifu Fransisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka huu,
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kukabiliana
kikamilifu na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa utandawazi
usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.
Baba
Mtakatifu anawataka waamini kujifunga kibwebwe ili kupambana dhidi ya
tabia ya uchoyo na ubinafsi, inayoendelea kujitanua kiasi hata cha
kupata mwelekeo wa kimataifa, kwa kuwabeza watu wanaoteseka, uwepo wa
ukosefu wa misingi ya haki na amani.
Ni tabia inayotaka kumwondoa
Mwenyezi Mungu katika maisha ya watu na kusahau kwamba, Mungu ameupenda
ulimwengu kiasi hata cha kumtoa Mwanaye wa pekee kwa ajili ya kumkomboa
mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu
Fransisko anasema kwamba, ni dhamana na jukumu la Kanisa kuhakikisha
kwamba, linaacha malango wazi ya mawasiliano kati ya Mwenyezi Mungu na
binadamu, kwa njia ya mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu,
Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, Ushuhuda wa imani tendaji
inayomwilishwa katika matendo ya huruma. Hata pale ulimwengu unapotaka
kujifungia na hatimaye kufunga lile lango na mawasiliano kati ya Mungu
na ulimwengu, Mwenyezi Mungu bado anaendelea kuonesha jitihada za
kumtafuta mwanadamu ili aweze kumwonjesha huruma na upendo wake usiokuwa
na kifani.
Kwaresima anasema Baba Mtakatifu, ni kipindi cha
mabadiliko, toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha Watu wa Mungu
kushinda kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko
ya watu na badala yake, kujenga utandawazi wa upendo, udugu na
mshikamano wa dhati.
Baba Mtakatifu anafafanua mambo mambo makuu
matatu yanayopaswa kufanyiwa kazi na Watu wa Mungu ili kuhakikisha
kwamba, wanataabikiana na kusumbukiana katika shida na mahangaiko yao,
kwani kama kiungo kimoja kinateseka, basi viungo vingine vyote
vinateseka pamoja nacho. Huu ni wajibu ambao kwanza kabisa unapaswa
kutekelezwa na Kanisa la kiulimwengu, kwa kuonesha umoja wa watakatifu
na katika mambo matakatifu.
Upendo wa Mungu ni silaha madhubuti
dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu,
ushuhuda wa upendo unaoneshwa na Mama Kanisa kwanza kabisa katika
maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hapa waamini wanakirimiwa
neema na baraka ya kuwa ni Ekaristi, yaani Mkate uliomegwa kwa ajili ya
jirani zao na hivyo kuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo,
yaani Kanisa, hapa ubinafsi na uchoyo havina nafasi tena!
Hatua ya
pili katika hija hii ya kipindi cha Kwaresima ni changamoto inayotolewa
na Baba Mtakatifu Fransisko katika dhamana na maisha ya Parokia na
Jumuiya zake, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linalosafiri hapa duniani,
linaunganika na lile Kanisa la Mbinguni, kwa kuungana pamoja katika
sala, huduma na mafao ya wengi, ili kuonesha utukufu wa Mungu. Waamini
pia wanapaswa kutambua dhamana na wito wao wa kimissionari, kwa kuvuka
mipaka inayowahusianisha na jamii inayowazunguka, tayari kwenda
kuwatangazia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, Habari
Njema ya Wokovu.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Fransisko kwamba,
Parokia na Jumuiya za Kiparokia ndipo mahali muafaka ambapo Kanisa
linaonesha kwa namna ya pekee kabisa utambulisho wake, kwa kuwa ni
visiwa vya huruma na upendo wa Mungu kati ya watu wanaozungukwa na
bahari kubwa ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema akisema
“imarisheni mioyo yenu”. Ni jambo la kutisha kabisa kuona jisni ambavyo
mwanadamu hana nguvu ya kupambana na mateso pamoja na mahangaiko ya
binadamu yanayoendelea kujitokeza kila siku siku ya maisha; lakini
wanaweza kuyashinda yote haya kwa njia ya mshikamano wa sala za wengi.
Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu anawaalika kuungana na Kanisa
zima, kwa ajili ya kumtolea Mwenyezi Mungu sala na maombi kwa musa wa
masaa 24, tukio litakalofanyika tarehe 13 na tarehe 14 Machi 2015.
Licha
yak usali, waamini wanahamasishwa kuonesha ushuhuda wa upendo kwa njia
ya matendo ya huruma kama kielelezo makini cha ushiriki wao katika
kuwashirikisha wengine upendo unaoguswa na mahangaiko ya jirani. Baba
Mtakatifu anasema kwamba, haiwezekani kwa mwamini kujiokoa peke yake,
kwani hiki ni kishawishi cha shetani. Hapa kunahitajika kama anavyosema
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI mchakato wa majiundo ya moyo
unaotambua umaskini wake na hivyo kujisadaka kwa ajili ya wengine.
Baba
Mtakatifu Fransisko anahitimisha ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka
2015 kwa kumwomba Yesu Kristo ili aweze kuifanya mioyo ya waamini
kufanana na Moyo wake Mtakatifu, unaosheheni nguvu na huruma; moyo
unaokesha na kuonesha ukarimu, ili usije ukatumbukia katika utandawazi
usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu. Kwa ujumbe huu, Baba
Mtakatifu anawatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Kwaresima
yenye mabadiliko na mafanikio makuu katika maisha ya kiroho!
|
No comments:
Post a Comment