DOM LAND BLOG

DOM LAND BLOG

Monday, February 02, 2015

OKWI AWAAHIDI MASHABIKI WA SIMBA MAMBO MAKUBWA

BAADA ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu juzi Jumamosi, straika wa Simba, Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, ameibuka na kuwaahidi makubwa mashabiki wa timu hiyo katika mechi zinazofuata huku akiwapooza kuhusu matokeo mabovu yaliyopita.
Okwi alipata fursa ya kuwaambia maneno hayo ya kuwatia moyo mashabiki hao baada ya kumalizika kwa mchezo wao huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar ambapo akiwa anatoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa ajili ya kupanda gari lake aondoke, aliwakuta mashabiki nje wakimsubiri kwa ajili ya kumlaki na ndipo mashabiki hao walipoanza kumshangilia na kumtaka aendelee kuitumikia timu hiyo kwa moyo wake wote kama anavyofanya sasa.
Okwi aliyekuwa akiongozana na Mganda mwenzake, Dan Sserunkuma alishangazwa na hali hiyo lakini baadaye akaonekana kufarijika kwa tukio hilo na ndipo alipoanza kuzungumza nao kuwa hawatakiwi kuvunjika moyo kutokana na kipindi kigumu walichokuwa wanakipitia nyuma kwani sasa timu hiyo ipo sawa na wataendeleza ushindi kwa kadiri watakavyoweza kwenye mechi zijazo.
Mashabiki hao waliokuwa wamemzunguka mchezaji huyo, walionyesha kufurahishwa na maneno hayo huku wakipiga shangwe na vifijo na kuendelea kupiga mayowe ya furaha huku wakimsindikiza kwenye gari lake.Katika mechi hiyo, Okwi ndiye aliyetengeneza nafasi zilizozaa mabao hayo mawili yaliyowekwa kimiani na Dan Sserunkuma.
"Hatukutakiwa kuvunjika moyo wakati ule, kila mchezaji ilikuwa inamuuma kuona tunapoteza mechi na kuwakera mashabiki lakini sasa timu ipo sawa na kila mchezaji yupo safi kwa ajili ya kupambana kuutafuta ushindi kwenye mechi zilizobaki.
"Tutahakikisha tunajituma kwa nguvu zetu zote katika hilo, ila tunaomba ushirikiano wenu pia," alizungumza Okwi na mashabiki hao na kisha kuingia ndani ya gari lake ambapo mashabiki walianza kulisukuma huku wakishangilia.
Kabla ya Okwi kuondoka uwanjani hapo, akimsubiri mchezaji mwenzake, Mganda, Simon Sserunkuma, mashabiki walitumia fursa hiyo kulifuta vioo gari lake na kulisafisha sehemu nyingine pia zilizokuwa na vumbi.
Lakini baada ya Simon kuja eneo hilo na kuingia ndani ya gari ndipo Okwi akaomba mashabiki wakae pembeni ili aondoe gari kwa ajili ya kwenda kupumzika na mashabiki wakampisha kwa roho safi.
Hali hiyo ni tofauti na ile iliyojitokeza kwenye mchezo wa Jumatano iliyopita, Simba ilipochapwa mabao 2-1 na Mbeya City ambapo mashabiki walionekana kuwa na jazba huku wakitaka kulipiga mawe basi la Simba, kabla ya polisi wa kutuliza ghasia kuingilia kati na kuanza kurusha mabomu ya machozi kwa ajili ya kutawanya umati uliokuwa nje ya uwanja huo. Picha ni kwa hisani ya Globalpublishers.


No comments:

Post a Comment