Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI Mh. Hawa Ghasia akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo pichani)
kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali ikiwemo kuwasimamisha kazi
baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali hapa nchini na wengine
kutenguliwa kwa uteuzi wao kutokana na kushindwa kusimamia vyema
uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mapema hivi karibuni kote
nchini. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Jumanne Sagini, Kulia ni
Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Bw. Kagyabukama Kilima.
Frank Mvungi- Maelezo
Serikali
yatengua uteuzi wa Wakurugenzi sita (6) wa Halmashauri mbalimbali hapa
nchini walioshindwa Kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mujibu
wa Sheria na Kanuni za Uchaguzi huo.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Hawa Ghasia wakati wa mkutano na Waandishi wa
Habari jana Jijini Dar es salaam uliolenga kutoa taarifa ya hatua
mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kwa wale wote walisababisha
kasoro mbalimbali katika uchaguzi huo.
Akitaja
majina ya Wakurugenzi ambao uteuzi wao umetenguliwa Mhe. Ghasia amesema
kuwa ni Bw. Benjamin A. Majoya ambaye Alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Mkuranga, Bw.Abdalla Ngodu Mkurugenzi Mtendaji Kaliua, Bw. Masalu Mayaya
Mkurugenzi Mtendaji Kasulu, Bibi Goody Pamba Mkurugenzi Mtendaji
Serengeti, Bw.Julius A. Madiga Mkurugenzi Mtendaji Sengerema na Bw. Simon
C.R. Mayeye Mkurugenzi Mtendaji Bunda.
Akizungumzia
wakurugenzi waliosimamishwa kazi Mhe. Ghasia amesema ni watano (5) ili
kupisha uchunguzi Zaidi wa Kiwango cha ushiriki wao katika kasoro
zilizojitokeza kwenye Halmashauri zao ambao ni Bw. Felix T. Mabula wa
Hanang, Bw. Fortunatus Fwema wa Mbulu,Bibi Isabella D. Chilumba wa
Ulanga,Bibi Pendo Malabeja wa kwimba na Bw. Wiliam Z. Shimwela wa
Manispaa ya Sumbawanga.
Kwa
upande wa Wakurugenzi waliopewa Onyo Kali na ambao watakuwa chini ya
uangalizi kubaini kama wana udhaifu mwingine ili wachukuliwe hatua zaidi
Mh. Ghasia amesema kuwa ni watatu (3) ambao ni Bw. Mohamed A. Maje wa
Rombo, Bw. Hamis Yuna wa Busega,Bw. Jovin A. Jungu wa Muheza.
Pia
Mh. Ghasia aliwataja wakurugenzi watatu (3) waliopewa onyo na kutakiwa
kuongeza umakini wanapotekeleza majukumu yao ambao ni Bw. Isaya Mngulumi
Manisapaa ya Ilala,Bw. Melchizedeck Humbe Humbe wa Hai na Bw. Wallace
J. Karia wa Mvomero.Akitoa
Wito kwa watumishi wa Umma na Viongozi wa Sekta ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa Mhe. Ghasia amesema kila mmoja anao wajibu wa
kutekeleza kwa weledi na uadilifu ili kuepuka kasoro zinazoweza
kuepukwa.
Ofisi ya
Waziri Mkuu TAMISEMI ilitimiza wajibu wake wa kuhakikisha uchaguzi wa
Serikali za Mitaa unafanyika kwa ukamilifu kwa kutoa miongozo na mafunzo
kwa watendaji wa Halmashauri ambapo Mikoa na Halmashauri ziliwezeshwa
kwa fedha ili kugharimia maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na kuandaa
vifaa na karatasi za kupiga kura. Chanzo: Mjengwa Blog
| | |
No comments:
Post a Comment