Wabunge
wa Kenya wametofautiana bungeni kufuatia mjadala kuhusu mswaada
tatanishi wa usalama ambao wabunge wa upinzani wanasema unakiuka uhuru
wa wakenya.
Bunge
lililazimika kuahirisha vikao vyake kwa dakika 30 badala ya kujadili
mswada huo. Kikao cha leo kilikuwa kikao
maalum ambacho kilipaswa kupitisha mswada huo ambao baadaye
utaidhinishwa na Rais kuwa sheria.
Wabunge wa upinzani walipinga mswada huo na kuanza kurusha karatasi sakafuni huku wakitatiza shughuli bungeni humo.
Mwenyekiti
wa kamati ya usalama wa bunge, Bwana Asman Kamama, alijaribu kuyajadili
mabadiliko yaliyopendekezwa kufanyiwa mswada huo lakini wabunge walianza
kuimba na kumzomea Spika wa Bunge wakiukataa mswada huo wakisema 'bado
mapambano'.
Spika wa Bunge Justin Muturi wakati mmoja aliamuru walinzi wa bunge kuwaondoa
baadhi ya viongozi waliofika bungeni humo kwa mjadala ambao ulitarajiwa
kuwa kaa la moto, hasa kwa upande wa upinzani.
Mswada
huo ambao umewasilishwa bungeni kufuatia matukio ya utovu wa usalama na
mashambulizi nchini Kenya, unapendekeza kuwa washukiwa wa ugaidi wanaweza
kuzuiliwa kwa mwaka mmoja huku polisi wakifanya uchunguzi.
Mapendekezo ya mswada huo ni kwamba mshukiwa wa ugaidi anaweza kuzuiliwa kwa siku 360 kutoka siku 90 za awali.
Pia, ikiwa
mswada huo utapitishwa kuwa sheria, mashirika ya habari yatatozwa faini
ya shilingi milioni 5 kwa kuchapisha taarifa au picha ambazo
zinaleta hofu na kusababisha taharuki nchini humo.
Mswada
huu umetolewa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na wapiganaji wa Al-Shabaab wakilalamika na kutaka wanajeshi wa Kenya kuondolewa Somalia.
Rais
Kenyatta amekuwa akikabiliwa na shinikizo kuimarisha usalama wa tangu
mashambulizi ya Septemba mwaka 2013 katika jengo la maduka ya kifahari
la Westgate mjini Nairobi ambapo watu 67 waliuawa.
|
No comments:
Post a Comment