Katibu wa itikadi na uenezi CCM Nape Nnauye.
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM), kimesema vitendo vinavyofanywa na Mbunge wa Monduli
na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ni ukiukwaji wa Katiba na
kanuni za chama hicho.
Aidha,
kimesema vitendo vinavyofanywa na Lowassa ni kampeni za wazi za urais
anazoendesha kabla ya muda kufika na hivyo kukiuka Katiba na kanuni za
CCM na kuonya kuwa kama ataendelea na kampeni hizo haramu atapoteza sifa
za kugombea nafasi ya urais.
Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alitoa ufafanuzi huo baada ya
waandishi wa habari waliopo katika msafara wa Katibu Mkuu wa CCM,
Abdulrahman Kinana kutaka ufafanuzi wa kinachoendelea mjini Dodoma kwa
makundi tofauti kwenda kwa Lowassa kwa madai ya kumshawishi agombee
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nape
akizungumzia suala hilo alisema, “Anachokifanya Lowasa ni kuvunja kanuni
na kiburi, ni matendo ya wazi ya kampeni, bila shaka anajua adhabu
yake. Matendo hayo yanaweza kumpotezea sifa za kuwa mgombea kupitia
CCM.”
Katibu
huyo wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa aliongeza kuwa Lowassa ni miongoni
mwa wanaCCM ambao walipewa adhabu na CCM mwaka mmoja uliopita kwa kuanza
kampeni kabla ya wakati na mpaka sasa bado wapo kwenye kipindi cha
uangalizi wakati vikao husika vikiendelea na tathmini dhidi yao.
Nape alisisitiza kuwa matendo yanayoendelea hivi sasa ni dhahiri kuwa ni kiburi kisicho na maana dhidi ya CCM.
“Lowasa
anajua utaratibu wa Chama katika kuwapata wagombea wake kwa ngazi
mbalimbali kuanzia udiwani mpaka urais hivyo kuendelea na matendo ambayo
yanatafsiri ya wazi kuwa ni kampeni ni kiburi cha wazi. “Kwa matendo
hayo ya Lowassa labda dhamira iwe ni kuomba ridhaa ya kuwania nafasi ya
Urais kupitia chama kingine na si CCM.”
Nape
alisema ni vyema wagombea wa ngazi mbalimbali wakahakikisha wanazingatia
Katiba na kanuni za chama hicho ili wasiingie kwenye kundi la kutokuwa
na sifa ya kuomba ridhaa ya kugombea udiwani, ubunge na urais.
“Tunaendelea
kukumbusha na kusisitiza kwamba wale wote wenye nia ya kugombea kupitia
chama chetu kuheshimu kanuni na tararibu za kupata ridhaa kugombea kwa
ngazi ya chama chetu,” alisema Nape.
Lowassa
amedaiwa kuwa amekuwa akitumia makundi mbalimbali kufanya kampeni ambapo
alianza na kikundi cha wajasiriamali jimboni Monduli mkoani Arusha
ambapo walienda nyumbani kwake kumuomba agombee.
Hatua
hiyo ilifuatiwa na mashehe 50 kutoka wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani
ambao nao walikwenda nyumbani kwa Lowassa Dodoma kwa lengo la
kumshawishi agombee urais.
Baadaye
walifuata wachungaji ambao nao walifunga safari hadi nyumbani kwa
Lowassa Dodoma na kusema wameamua kumuomba Lowassa agombee urais kwa
madai kuwa ana maono makubwa dhidi ya Tanzania.
Baadhi ya
wachungaji hao walimwambia Lowassa wanaamini kuwa yeye ndio chaguo
sahihi kwao na ndio maana wameamua kufunga safari na kumshawishi huku
wakieleza kuwa kila mtu ametumia nauli yake kufika Dodoma.
Kwa
upande wake Lowassa, akizungumza na wachungaji hao waliofika nyumbani
kwake, alisema anafarijika kuona makundi mbalimbali yakifika nyumbani
kwake kumshawishi agombee.
Alinukuliwa
na vyombo vya habari juzi akisema pia kuwa hakuna kundi ambalo
analituma au kulipa fedha kwa ajili ya harakati za kutaka kugombea
urais.
Hata
hivyo, tayari baadhi ya makada wa CCM ambao wamo kwenye orodha ya kutaka
kugombea urais, wametoa malalamiko yao kuwa kinachofanywa na Lowassa si
sahihi.
Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema
kuwa kitendo cha kuandaa watu kwa ajili ya kuanza kampeni si cha
kiungwana na kwamba kila mgombea anaweza kufanya hivyo, lakini
wanaheshimu kanuni na Katiba za chama chao.
January
amenukuliwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii
akieleza wazi kuwa anaweza kutengeneza makundi kwa ajili ya kuonesha
Watanzania kuwa anahitajika, lakini akasema hizo ni propaganda ambazo
hazina tija kwa Taifa.
“Kama
mgombea anakubalika kwa Watanzania kwanini atumie fedha nyingi kutafuta
makundi ili aonekane anakubalika? Alihoji January katika ujumbe wake
aliousambaza katika mitandao mbalimbali ya kijamii. CHANZO: HABARI LEO
|