Nashukuru wote ambao mmekuwa
mkifuatilia hatma ya muswada binafsi wa Baraza la Vijana la Taifa
niliouwasilisha tarehe 31 Oktoba 2013.
Vijana na wadau wa maendeleo ya vijana
mzingatie kwamba muswada huo hatimaye umepangwa kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa
Bungeni Jumanne tarehe 31 Machi 2015 katika Mkutano wa 19 wa Bunge.
Muswada huo ulisomwa kwa mara ya
kwanza katika Mkutano wa 14 wa Bunge tarehe 21 Disemba 2013. Maoni kutoka kwa
wadau yalikusanywa Oktoba 2014 na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya
Jamii.
Baraza la Vijana la Taifa pamoja na
malengo mengine litawezesha vijana kuanzia kwenye vijiji/mitaa mpaka taifa
kuweza kuwa na vyombo vya kuwaunganisha vijana kwa kike na wa kiume kwa ajili
ya maendeleo yao na ya taifa.
Aidha, Baraza hilo litafuatilia pia
kwa karibu utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya vijana ikiwemo kuhusu ajira,
elimu na sekta zingine katika Halmashauri, Serikali kuu, katika vyombo mbalimbali
vya maendeleo na wadau wa maendeleo.
Pia, Muswada huo utawezeshwa
kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kulipa jukumu Baraza la Vijana
kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana; kuhakikisha
kwamba fedha zinatengwa za kutosha na kufika kwa walengwa kuwawezesha vijana
kujiajiri, kukuza vipaji vyao na kushughulikia maendeleo yao kwa ujumla.
Kujadiliwa kwa muswada huo ni hatua
ya pekee katika historia ya harakati za vijana nchini kwa kuzingatia kuwa Sera
ya zamani ya maendeleo ya vijana ya mwaka 1996 ilitamka kwamba
kutaanzishwa Baraza la Vijana na suala
hilo kurudiwa katika Sera mpya ya mwaka 2007.
Hata hivyo Serikali imekuwa ikikwepa
kuhakikisha kwamba matakwa hayo ya sera tajwa yanatekelezwa kwa wakati pamoja
na kuwa suala hilo linahusu mustakabali wa maendeleo ya vijana nchini.
Natambua mchango wa vijana na
taasisi zote za vijana mlioshiriki katika maandalizi ya muswada huu, unaitwa
binafsi kwa sababu tu ndio neno linalopaswa kutumika kwa mujibu wa Kanuni za
Bunge lakini ukweli ni kwamba huu ni muswada wenu; mimi ni mwakilishi.
John Mnyika (Mb)
Machi 2015
|
No comments:
Post a Comment