Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa katika moja ya mikutano ya kujadili masuala ya uchumi
Rais
mstaafu Benjamin Mkapa amesema sekta ya uwekezaji nchini inashindwa
kukua kwa kasi inayotarajiwa kutokana na baadhi ya wanasiasa
kutokuielewa vizuri.
Akizungumza
leo wakati wa kusaini makubaliano ya kusaidia kuvutia na kuongea
uwekezaji wa ndani na nje nchini kati ya Taasisi inayoshughulikia
mazingira ya uwekezaji Barani Afrika (ICF) na Kituo cha Uwekezaji nchini
(TIC), Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa ICF alisema baadhi ya
watu wanautazama uwekezaji kama unyonyaji.
"Watu wanaona wanataka kunyonywa na sio kunyonyana," alisema Mkapa wakati akielezea mafanikio ya TIC tangu kuanzishwa kwake.
Chini ya
makubaliano hayo yaliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa ICF, William
Asiko na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Juliet Kairuki, ICF itakisaidia
kituo cha uwekezaji nchini kukuza, kuinua na kulingaza dirisha la
uwekezaji na kuimarisha uwezo wake katika kuwezesha na kufuatilia
uwekezaji nchini.
Kairuku
alisema Dola 950,000 (Sh1.7 bilioni) zitatolewa kwa ajili ya mradi wa
dirisha la uwekezaji Tanzania ambazo zitachangwa kwa pamoja kati ya ICF
na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kurahisisha huduma zote
zinazotolewa TIC kupatikana haraka, kwa ufanisi na bila kupoteza muda.
"Huduma
zote zinazotolewa na TIC sasa zitakuwa zikipatikana mtandaoni ikiwa ni
pamoja na kulipia ada mbalimbali, tunajaribu kuwa wa kisasa," alisema
Kairuki na kuongeza kuwa huduma hiyo itawanufaisha zaidi wawekezaji wa
mikoani.
Mpango
huo unatarajiwa kuwapa wananchi nafasi ya kupata huduma zote za kituo
hicho kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Idara ya
Uhamiaji, Wizara ya Ardhi, Mamlaka ya HIfadhi za Jamii (SSRA) na Wakala
wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) kwa kutumia mfumo wa
kieletroniki.
Mwenyekiti
mwenza wa ICF, Neville Isdell alisema uwekezaji unahitaji uwazi ili
kuwavutia wafanyabiashara wa ndani na nje kuendelea kuwekeza.
"Biashara
zote hususani zilizo ndogo zinahitaji kuwa na mazingira yaliyo mazuri
watakayofanyia shughuli zao. Kwa kuwa na dirisha la uwekezaji biashara
nyingi zitaweza kukua, kuongezeka na kushamiri haraka," alisema Isdell.
Waziri wa
Uwekezaji na Uwezeshaji, Christopher Chiza alisema mradi huo
utakapokamilika utasaidia kuboresha mazingira ya biashara na ushindani
nchini.
"Kwa muda
wa miaka michache iliyopita nafasi ya Tanzania kimataifa katika kufanya
biashara kwa mujibu wa ripoti mbalimbali imekuwa hairidhirishi, ishara
ambayo sio nzuri kwa wawekezaji na sekta binafsi," alisema Chiza.
|
No comments:
Post a Comment