Rais
Jakaya Kikwete akikagua gwaride maalumu wakati wa hafla ya kuwatunukia
vyeo maofisa 289 wa Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini
jijini Dar es Salaam
Rais
Jakaya Kikwete amelikata Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili
kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji
wapigakura, upigaji Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Akifunga
mafunzo ya maofisa warakibu wasaidizi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi,
Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna
watu wenye nia ya kuhatarisha amani katika matukio hayo.
"Tunayoyasikia
na tunayoyaona yanaashiria kuwapo kwa dalili za wenzetu kukwamisha
shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni
na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa lengo la kuhatarisha amani,"
alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa yaliyowasilishwa kwake na Mkuu
wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.
Alisema
Serikali itahakikisha kazi ya uandikishaji katika daftari la wapigakura,
upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu vinafanyika kwa amani na
utulivu kwa gharama zozote.
Alisema
ili kufanikisha kazi hiyo, Serikali italiwezesha Jeshi la Polisi ili
litekeleze kikamilifu majukumu yake ya kulinda amani na utulivu.
"Tutawawezesha
kwa kuwapa vifaa ili kuhakikisha mnafanya kazi yenu ya kutunza amani
kwa umakini zaidi," alisema Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula
miwili ya urais baada ya uchaguzi mwaka huu.
Iwapo
mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Kura ya Maoni ya Katiba
Inayopendekezwa itapigwa Aprili 30 wakati Uchaguzi Mkuu utafanyika
Oktoba.
Profesa Lipumba apinga.
Akizungumzia
kauli hiyo ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
alisema, "Rais Kikwete yeye ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa
kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake
na jukumu hilo ni la NEC, Serikali yake kushindwa kuratibu vyema
mchakato wa uandikishaji.
"Kama
uandikishaji hauendi vizuri mpaka sasa, anavunja sheria za nchi halafu
yeye mwenyewe tena anakwenda kwa vyombo vya dola na kuvieleza vijiandae
wakati yeye huyohuyo ndiye ameanzisha uvunjifu wa amani tunashindwa
tumweleweje," alisema.
Profesa
Lipumba alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni NEC kutangaza tarehe
kamili ya uchaguzi na uandikishaji uende kwa utaratibu tofauti na
ilivyo sasa kwa mkoa mmoja wa Njombe kusuasua mambo ambayo yanaashiria
uvunjifu wa amani. CHANZO: MWANANCHI.
|
No comments:
Post a Comment