Tunawaunga
mkono wabunge waliojitokeza kupinga kuwasilishwa kwa hati ya dharura
muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa mwaka 2015.
Wakizungumza
bungeni juzi, baadhi ya wabunge waliihoji Serikali sababu ya
kuharakisha kuwasilisha muswada huo kwa ajili ya kupitishwa kama sheria.
Si
wabunge pekee, wadau wa sekta ya habari wanajiuliza kuhusu uharaka wa
muswada huo ambao kimsingi si suala la jana au juzi. Ni suala la muda
mrefu ambalo wadau wa habari wamekuwa wakilipigania.
Ikiwa
muswada huu utawasilishwa kwa njia ya hati ya dharura, ina maana
utasomwa kwa mara ya kwanza na kupitishwa vipengele vyote kwa siku moja.
Hii ina maana kuwa si wadau wa habari wala watunga sheria wetu,
watakaopata muda wa kutosha wa kuupitia muswada na kujiridhisha kuwa una
kila sababu ya kuwa sheria kwa maendeleo ya sekta ya habari na
wanahabari.(P.T)
Aidha,
wadau wa habari kama wataalamu wa sekta hiyo, watakosa fursa ya
kuwaelewesha wabunge masuala mbalimbali yaliyomo katika muswada, ili
hata wanapoupitia wawe na weledi wa kutosha wa kitu wanachotaka
kukipitisha kuwa sheria rasmi.
Mchakato
mzima wa suala hili umegubikwa na usiri ambao sisi tukiwa wadau wa
habari, unatupa wasiwasi na hata kujiuliza una maana gani? Nini
kimejificha nyuma ya usiri huu?
Tumesema
hapo awali hili si suala la jana wala juzi, tumekuwa tukilipigania kwa
muda mrefu. Kwa nini taratibu za kawaida za uwasilishaji wa miswada
zisifuatwe ili wadau wote wajiridhishe kuwa sheria itakayotungwa itakuwa
na tija na maendeleo kwa sekta yenyewe, wanahabari na Taifa kwa jumla?
Kinachotokea
sasa kuhusu haraka na usiri ulioligubika suala hili, wadau wa habari
hasa wanahabari wanaweza kusukumwa kuamini kuwa kuna dhamira isiyo njema
kwao.
Hofu hii
ya wanahabari imeshaanza kujidhihirisha katika mjadala bungeni, baada ya
baadhi ya wabunge kufikia hatua ya kuinyooshea kidole Serikali kuwa
pengine ina dhamira ya kutaka kuvikandamiza vyombo vya habari kupitia
muswada huo.
Hatutaki
kuamini kuwa Serikali yetu sikivu na inayoongoza kwa misingi ya
kidemokrasia, inaweza kutunga kwa makusudi sheria inayolenga kuvibana
vyombo vya habari. Na kama itakuwa hivyo, tunauliza ni kwa masilahi ya
nani?
Tunawakumbusha
viongozi na watendaji serikalini kuwa Tanzania ni nchi yetu sote,
hakuna mtu mwenye haki ya kujiona yeye ni Mtanzania zaidi kuliko wengine
au mzalendo kuliko wengine.
Tunatoa
tanbihi hii kwa kuwa umejengeka utamaduni wa viongozi serikalini na hata
wanasiasa kufikiri kuwa wao ni weledi wa kila kitu kuhusu maendeleo na
ustawi wa Taifa hili. CHANZO: MWANANCHI
|
No comments:
Post a Comment