Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras
Mazungumzo ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Waziri Mkuu wa
Ugiriki, Alexis Tsipras, yamemalizika huku kukiwa na dalili ndogo za
kupatikana suluhu ya mvutano uliopo kuhusu mpango wa uokozi wa Ugiriki.
Kansela Merkel na Tsipras walikuwa na mazungumzo ya kina yaliyodumu kwa
muda wa saa tano mjini Berlein, ambayo yameonekana kuwa ya kujenga
katika mazingira ya kirafiki, huku wakisisitiza nia yao ya kuondoa
mvutano uliopo kati ya serikali zao. Viongozi hao wamezungumzia kuhusu
hali ya kiuchumi ya Ugiriki, utaratibu wa Umoja wa Ulaya na mustakabali
wa ushirikiano kati ya Ugiriki na Ujerumani.
Akizungumza katika mkutano wake na Tsipras na waandishi wa habari,
Merkel amesema licha ya tofauti zilizopo sasa kuhusu mpango wa uokozi
kuisaidia Ugiriki isifilisike kiuchumi pamoja na masuala mengine kadhaa,
nchi zao zimeendelea kubakia washirika wa karibu, huku wakiwa na
uhusiano mzuri kisiasa na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni
muhimu.
''Nataka kusisitiza wazi kuwa Ujerumani ina uhusiano wa karibu na
kirafiki na Ugiriki pamoja na watu wa Ugiriki. Kuna watu wengi wanaoishi
Ujerumani ambao wana asili ya Kigiriki,'' alisema Merkel.
Kwa upande wake Tsipras ambaye anazuru rasmi Ujerumani kwa mara ya
kwanza tangu aingie madarakani mwezi Januari mwaka huu, ameonyesha kuwa
nchi yake bado inatafuta masharti nafuu yatakayosaidia kuunusuru uchumi
wake.
Tsipras kuzingatia mafanikio yaliyopatikana
''Hatutaki kuharibu mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita.
Tunahitaji kutekeleza mageuzi ambayo awali serikali zilizotangulia,
zilishindwa kuyafikia, mageuzi ya kodi, hatua za kupambana na rushwa
pamoja na ukwepaji wa kulipa kodi,'' alifafanua Tsipras.
Uhusiano kati ya Ujerumani na Ugiriki uliingia dosari tangu Tsipras na
serikali yake inayoongozwa na chama cha Syriza kuingia madarakani na
kuendeleza sera yake ya kupinga vikali masharti magumu ya kubana
matumizi.
Kansela Merkel amesema uamuzi wowote kuhusu suluhisho la matatizo ya
kifedha yanayoikumba Ugiriki utapatikana tu kutoka kwa mataifa yote
yanayotumia sarafu ya Euro. Wiki ijayo serikali mpya ya Ugiriki
inatarajia kuwasilisha orodha yake ya mageuzi ya kiuchumi.
Asubuhi hii, Tsipras atakutana na viongozi wa chama cha upinzani cha
siasa kali za mrengo wa kushoto-Die Linke, Katja Kipping na Gregor Gysi,
ambapo majira ya mchana anatarajiwa kukutana na viongozi wa chama cha
Kijani, Cem Ă–zdemir na Simone Peter.
Baadae, waziri huyo mkuu wa Ugiriki, atatembelea makumbusho ya mauwaji
yaliyofanywa na utawala wa Wanazi dhidi ya Wayahudi, Holocaust mjini
Berlin, hatua ambayo inaelezwa huenda ikatilia mkazo madai ya serikali
yake ya kutaka kulipwa fidia, ambayo Tsipras ameyaita kama ''suala la
kimaadili.''
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
|
No comments:
Post a Comment