Na Mwandishi Wetu
…………………………………….
MKOA wa Kigoma ni hazina kubwa
ya vipaji hapa nchini Tanzania. Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi
toka mkoani humo hasa vya wanamichezo na wasanii. Mfano kwa upande wa
kandanda tutaona kwamba mkoa huo ulitingisha kwa vipaji vya wanasoka.
Kina Manara, Kitwana Manara,
Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu zao wengine wanatoka Kigoma.
Baadaye kikafuatia kizazi cha kina Edbily Lunyamilla, Nteze John, Omari
Mavumbi, Itutu Kigi na wengineo wengi.
Kwa upande wa wasanii wa muziki
Kigoma imetoa watu wengi wenye majina makubwa katika sanaa hiyo, kama
Shem Karenga, Hassan Rehan Bitchuka, Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro,
Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota Waziri na wengineo wengi.
Kwa upande wa muziki wa kizazi
kipya Kigoma imetoa vijana wengi wa muziki huo wakiongozwa na mtaalamu
wa muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba, kucheza kila ala ya muziki na
kutengeneza muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo ‘Bizman’. Wapo wengine kama
Ally Kiba, Banana Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’ na wengineo.
Lakini pamoja na wote hao makala
hii ni mahususi kwa moja ya vipaji hivyo vya mkoa wa Kigoma ikiwa
imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi kipya kwa sasa hapa nchini,
Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.
Diamond kadhihirisha kipaji cha
sanaa ya muziki kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa muda mfupi
alioutumia katika sanaa. Hiyo ni tofauti na kipindi alichokitumia mfalme
wa muzuki wa POP duniani, Michael Jackson, kuwa kileleni mwa mafanikio
kwa zaidi ya miaka 10 kati ya 1967 – 1979.
Lakini ndani ya miaka mitatu
Diamond ameweza kuibeba Tanzania na kuiweka kwenye chati ya kimataifa
kwenye fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya. Na ninaposema ngazi ya
kimataifa sina maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za
jirani kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji
wala Kongo, kama ambavyo wameweza kufanya wasanii wengine wa muziki huo
wa hapa nchini, ninamaanisha kimataifa kwa maana halisi. Nalenga nchi za
mbali na Tanzania.
Muziki wa Diamond kwa sasa
unapigwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika, ukiondoa nchi za Kiarabu kwa
upande wa Afrika Kaskazini, ambako sina uhakika kama muziki wa kizazi
kipya una mashabiki kulingana na utamaduni wa huko.
Kwa maana hiyo Diamond kaiweka
Tanzania kwenye chati ya kimataifa kwa maana halisi kimuziki. Kwa sasa
msanii huyo anakula sahani moja na wasanii wa kimataifa kama kina Peter
Okoye na Paul Okoye, Wanigeria wanaounda kikundi cha P Square, ambao
mara kadhaa wamemuomba watoe naye vibao vya pamoja. Pia yuko kwenye
kiwango cha wanamuziki kama Youssou N’Ndour wa Senegal na wengine wa
aina hiyo.
Kwa eneo hili la Afrika
Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond na Joseph Mayanja
‘Chameleone’. Kwa sasa wanamuziki hao wanafanana.
Tanzania iliwahi kuvuma sana
duniani miaka ya nyuma kupitia kwa wanamichezo, hususan wanariadha, kina
Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa mbio za mita 1500 duniani,
ambaye mpaka sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo kwenye michezo ya
Jumuiya ya Madola aliyoiweka mjini Christchurch nchini New Zealand mwaka
1974. Wengine ni Seleman Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa,
Gidmas Shahanga na wengine wengi.
Lakini kutokana na umri kuwatupa
mkono nyota hao, jina la Tanzania limefifia katika tasinia ya michezo
na kuifanya nchi yetu isahaulike kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja
ya michezo na burudani!
Hivyo Diamond ni kijana
aliyedhamiria kulipandisha tena jina la nchi yake kupitia tasnia ya
burudani. Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba ameweza. Hilo
linashadidiwa na tuzo mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa sasa kwa
upande huo wa burudani baada ya kushindanishwa na wasanii wengine wa
kimataifa toka nchi mbalimbali.
Kitu cha kipekee nilichokigundua
kwa Diamond na kuhisi kwamba pengine ndicho kinachochochea mafanikio
yake ni tabia yake ya kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi.
Wakati fulani nilimpa
changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa kwa Chameleone nilipokutana
naye Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba kwa kiwango alichopo hapaswi
kuendelea kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa “Play back”, kwamba
anatakiwa kuwa na vyombo vyake na kupiga muziki live. Diamond kanielewa
na kusema kwamba hilo analifanyia kazi kwa bidii kubwa.
Kingine ni namna anavyoendesha
mahusiano na jamii aliyomo. Kawaida kuna dhana ya kwamba wasanii ni watu
wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni na huo kuwa mwanzo wa neno
usanii, kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na maana ya kanifanyia
uhuni.
Lakini hilo ni tofauti kwa
Diamond. Yeye anapenda kuwasaidia wenye mahitaji kulingana na hali
halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa kuuthamini mchango wa Baba
wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Maalim Gurumo, aliamua kumpatia
gari jipya. Huo ni usanii kwa upande wa pili anaouonyesha Diamond
tofauti na upande uliozoeleka kwa jamii.
Diamond anasema kwamba
amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea vituo vya watoto yatima na kutoa
misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo ni mchango mwingine katika
jamii anaoufanya kijana huyo.
Anawashauri vijana wenzake, hasa
wasanii, wanaojiingiza kwenye ulevi uliopindukia pamoja na matumizi ya
dawa za kulevya waache mambo hayo mara moja. Anasema kwamba yanaharibu
vipaji na wakati mwingine kupoteza maisha. Anasema ili kulinda kipaji
chake yeye anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na maana na
yaliyo hatari kwa maisha ya binadamu.
Diamond anasema kwamba alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma.
Anasema kwamba kilichomfanya
aingie kwenye muziki ni kipaji chake kilichojitokeza tangu akiwa shule
ya msingi. alikuwa akiimba kwenye kwaya ya shule na burudani nyingine za
shuleni.
Huyo ndiye Diamond Platnumz,
ambaye wasanii wengine vijana wanapaswa wamtumie kama kipimo ya
mafanikio katika muziki wa kizazi kipya wanaoufanya. Bila shaka
watakaofuata mwenendo wake watafanikiwa kama yeye alivyo. CHANZO: FULLSHANGWEBLOG.COM
|
No comments:
Post a Comment