Rais Goodluck Jonathan, Nigeria.
Rais wa
Nigeria, Goodluck Jonathan amesema ana matumaini kuwa wanamgambo wenye
itikadi kali za Kiislamu wa Boko Haram watafurumushwa kutoka kwenye miji
na vijiji wanavyovidbihiti, katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.
Rais
Jonathan ameitoa kauli hiyo leo katika mahojiano yaliyorushwa na Kituo
cha Utangazaji cha Uingereza, BBC, wakati ambapo kundi la Boko Harama
likiwa limewaua watu 11 kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo. Watu
walioshuhudia wamesma wanamgambo wa Boko Haram wameshambulia mji wa
Gamboru uliko kwenye jimbo la Borno, Nigeria.
Wakaazi
wa mji wa Fotokol ulioko kwenye mpaka wa Cameroon na Nigeria, wamesema
shambulizi hilo limefanyika siku ya Jumatano, mwezi mmoja baada ya
Gamboru kutwaliwa tena na majeshi ya Chad, ambayo ni sehemu ya
operesheni ya kijeshi iliyoanzishwa na mataifa manne ya kanda hiyo,
dhidi ya Boko Haram.(P.T)
Mkuu wa
vikosi vya Niger katika operesheni za kupambana na Boko Haram, Kanali
Toumba Mohamed, anasema walikuwa na wakati mgumu wakati wa kupambana na
kundi hilo. ''Tulikabiliana na adui ambaye kweli alikuwa amelidhibiti
eneo hili na halikuwa jambo rahisi kumuondoa, lakini tumefanikiwa na
nguvu za huyu adui zimepungua,'' alisema Kanali Mohamed.
Mudi
Dankaka mkaazi wa Fotokol, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba
wanamgambo wa Boko Haram waliuvamia mji wa Gamboru ulioko mpakani mwa
Nigeria na Cameroon, wakiwa katika pikipiki na kuwaua watu wanane siku
ya Jumatano. Dankaka, amefafanua kuwa watu wengine watatu waliuawa jana
Alhamisi. Shambulizi hili linaonekana kama changamoto kubwa
zinazoikabili Nigeria wakati ikielekea kufanya uchaguzi wake mkuu hapo
Machi 28, mwaka huu.
Mwezi
uliopita, majeshi ya Chad yalipongezwa kwa kuukomboa mji wa Gamboru
kutoka kwa Boko Haram, lakini hatua ya majeshi hayo kuondoka Nigeria
wiki iliyopita, inaonekana kuuacha mji huo bila ulinzi wowote kutoka kwa
majeshi ya Nigeria.
Operesheni ina lengo la kuliteketeza kundi la Boko Haram
Operesheni
ya pamoja ya majeshi ya Chad, Nigeria, Cameroon na Niger ni sehemu ya
lengo la kuliteketeza kabisa kundi la Boko Haram ambalo limekuwa
likiendesha operesheni zake kwa miaka sita sasa. Siku ya Jumanne, jeshi
la Nigeria lilisema kuwa limewafurumusha wanamgambo wa Boko Haram kutoka
kwenye wilaya zote za kaskazini-mashariki.
Shambulizi
la Gamboru limefanyika baada ya kutolewa taarifa za ukatili mwingine
uliofanywa na Boko Haram katika mji wa Bama, ulioko pia kwenye jimbo la
Borno. Kundi hilo liliwachinja wanawake kadhaa ambao walilazimishwa
kuolewa na wanamgambo wake. Watu walioshuhudia wamesema magaidi hayo
walifanya ukatili huo, wakisema hawawezi kuwaruhusu wake zao waolewe na
wanaume makafiri. Msemaji wa usalama wa ndani wa Nigeria, Mike Omeri,
alisema atajaribu kuthibitisha kuhusu taarifa hizo.
Ama kwa
upande mwingine, balozi za Marekani katika mataifa ya Afrika Magharibi
ya Niger na Mali, zimeimarisha usalama wa wanadiplomasia wake pamoja na
familia zao, huku kukiwa na wasiwasi wa nchi hizo kushambuliwa na
wanamgambo wenye itikadi kali za Kiislamu, wakiwemo Boko Haram.
Hatua
hiyo inatokana na shambulizi la kigaidi lililofanywa Machi 7 kwenye
mkahawa mmoja huko Bamako uliokuwa na raia wengi wa kigeni, pamoja na
mashambulizi yaliyofanywa na Boko Haram nchini Niger.
Kundi la
Boko Haram ambalo linaendesha shughuli zake kaskazini mwa Nigeria,
limekuwa katika vita na Nigeria na mataifa jirani tangu mwaka 2009 na
limesababisha mauawaji ya zaidi ya watu 13,000.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo kwa msaada wa Mashirika ya Habari ya Kimataifa ya AFPE,RTRE,APE-DW
|
No comments:
Post a Comment