Hali
ni tete katika jiji la Dar es Salaam, kutokana na mvua ya masika
iliyonyeshwa kwa siku tatu na kusababisha vifo vya watu watano, huku
nyumba nyingi zikiwa zimezingirwa na maji.
Maeneo
yaliyoathirika zaidi ni Buguruni kwa Mnyamani na eneo la Jangwani katika
Manispaa ya Ilala, ambako nyumba nyingi na barabara zimeathirika.
Sehemu
nyingine za jiji zimezingirwa na maji kutokana na kuziba kwa mitaro na
mifereji, ikiwa ni athari ya utupaji taka ovyo na pia miundombinu duni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mvua kubwa zaidi zinatarajia kuendelea kunyesha mpaka Jumatano.
Kutokana
na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, Mkuu wa Mko wa Dar es Salaam,
Said Meck Sadiki (pichani) jana aliongoza kikosi cha uokoaji katika eneo
la Buguruni kwa Mnyamani, ambako nyumba 250 zilizingirwa na maji, jambo
ambalo vikosi vya uokoaji vililazimika kufanya kazi ya kuwanasua watu
waliokuwa wamekwama katika nyumba zao.
Uokoaji
huo ambao mpaka jana jioni ulikuwa ukiendelea, ulisaidiwa na wafanyakazi
wa kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE), inayojenga
Daraja la Kigamboni, kwa kutoa vifaa na kushiriki katika uokoaji wa watu
hao.
Sadiki
alisema mpaka jana mvua hizo zimesababisha vifo vya watu watano, akiwemo
mtu mmoja aliyesombwa na maji, mwingine aliyeangukiwa na ukuta na
watatu ambao wamenaswa na umeme baada ya nguzo ya umeme kuanguka Mbagala
Mzambarauni katika Manispaa ya Temeke.
"Wananchi
wanatakiwa kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo katika maeneo ya
mitaro, kwani ndiyo yaliyochangia maji kuleta madhara, na walio
mabondeni bado nawasihi kuondoka maeneo hayo," alisema.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema mtu mmoja ambaye
hajatambuliwa mwenye umri kati ya miaka 45 hadi 50, anasadikiwa kusombwa
na maji katika mto Goba.
Aidha,
alisema katika eneo la Mwananyamala, mlemavu wa viungo Edward Warioba
(22) aliangukiwa na ukuta usiku wa kuamkia jana akiwa amelala katika
nyumba iliyokuwa imeingia maji na kulowanisha kuta zake.
Wambura alitaka wananchi kuchukua tahadhari kwa watoto wao na wahakikishe wanakwenda na kurudi kutoka shule wakiwa salama.
Eneo la
Jangwani, kati ya Magomeni na Faya (Kariakoo), pia nyumba kadhaa
zilizingirwa na maji huku baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wakihamia
barabarani ili kujinusuru.
Lakini
eneo la Jangwani, karibu na klabu ya Yanga, walionesha kutokuwa na
wasiwasi na mvua zinazoendelea kwa madai kuwa hazijafikia kiwango cha
kuwa na athari kwao.
"Kipimo
chetu ni hiki hapa, (wanaonesha alama) maji yakifika kimo hiki tunajua
wakati wa kuhama nyumba zetu umewadia lakini kwa sasa maji haya hayana
madhara yoyote," alisema mkazi wa eneo hilo, Huseni Juma.
Akizungumza
jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk
Agnes Kijazi alisema mvua kubwa zaidi ya milimita 50 ambazo zimenyesha
sasa, zinatarajia kuendelea kunyesha ndani ya saa 24 zijazo huku mvua
hizo kuendelea kunyesha hadi Machi 25, mwaka huu.
"Utabiri
unaonesha kuwa mvua kubwa za zaidi ya milimita 50 zitaendelea kunyesha
siku tatu zijazo. Hivyo ni vema wananchi wakaendelea kuangalia utabiri
unaotolewa na mamlaka kila siku ili kujiepusha na madhara," alisema.
Awali,
TMA ilitoa mwelekeo wa mvua za masika kwa kipindi cha Machi, Aprili na
Mei na kuwa kipindi hicho mvua zilitarajiwa kuwa ya kuridhisha katika
maeneo mengi ya nchi.
|
No comments:
Post a Comment